2016-11-18 10:41:00

Ni Ufalme wa ukweli na uzima; Utakatifu na neema; Haki, mapendo na amani


Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Hii ni Sherehe inaangukia Dominika ya mwisho ya mwaka wa Kanisa wa Kiliturujia. Hii ina maana kwamba kuanzia Dominika ijayo tutakuwa tumeingia rasmi katika mwaka mpya wa kiliturujia, yaani Mwaka A wa Kanisa. Adhimisho la mwaka huu libeba sura ya kipekee kwa sababu kwa mwaka mzima tumekuwa tukisafiri pamoja huku tukiwa na nia ya kuitafuta, kujifunza na kuikumbatia huruma ya Mungu katika Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Ni nafasi ya pekee kufanya tathimini katika Sherehe ya leo na kuona jinsi Ufalme wa Kristo ulivyopatiwa nafasi katika maisha ya Kanisa na kwa namna ya pekee Kanisa linalojifunua katika kila nafsi ya mmoja wetu.

Tuanze kwa kuutafakari Ufalme wa Kristo ni wa namna gani. Katika kurasa za Injili Kristo anaulizwa juu ya ufalme wake. Jibu lake kwa mamlaka za kidunia zinautofautisha ufalme wake na tawala za ulimwengu huu: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa". (Yoh. 18:36). Hapa tunaona moja kwa moja akiutenganisha ufalme wake na siasa au maelekeo ya kidunia.

Tunasoma mahali fulani Kristo akijitofauitisha na watawala ambao wanatafuta kutawala kwa mabavu, wanaotafuta kutukuzwa, wanaotafuta kujiongezea wenyewe. Hapo Kristo aliwaonya Mitume kutofikiri utawala wake katika mrengo huo bali watambue kuwa utawala wake utakapokuja utawafanya wawe watumishi wa wale wanaowaongoza huku wakitoa huduma inayopambwa na upendo wa Mungu. Si ufalme unaolenga kutafuta kutawala sehemu fulani katika tawala za kiulimwengu bali ni utawala unaotaka kujidhihirisha katika maisha ya mwanadamu mzima na kuelekeza kutenda kwake na kufikiri kwake

Kristo anaendelea kujidadavua kwamba Ufalme wake ni kwa ajili ya kuutawadha ukweli: “Nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nilikuwa ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli Huisikia sauti yangu” (Yoh 18:37). Prefasio ya Sherehe ya leo inatufafanulia ukweli huo ambao Kristo amekuja kuushuhudia, ukweli ambao kama ukitawala katika jamii ya mwanadamu leo hii basi huruma ya Mungu itathibitishwa kwa wanadamu. “Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote”.  Ufalme wake unaongozwa na alama ya kwanza ya ukweli. Ukweli huu unamaanisha kuviweka viumbe vyote katika namna yake halisi na ilivyokusudiwa. Kristo kama anavyodokeza Mtume Paulo katika somo la pili la leo ni utimilifu wa viumbe vyote na pale tu vyote vinavyojifungamanisha naye ndipo amani hutawala. Ufalme wake unadhihirika katika kuyafanya yote kadiri ya mpango wa Mungu, yaani pale tunapomfanya Mungu kuwa yote katika yote.

Ufalme wa Kristo, utangulizi huo kuuelezea kama “Ufalme wa utakatifu na neema”. Ukweli huo ambao tunauchota katika Kristo unatufanya kuwa wakamilifu na bila hitilafu mbele ya Mungu. Mwanadamu anapoukumbatia ukweli huo humaanisha kwamba anaungana na Kristo ndani yake na kadiri ya ahadi yake anakuwa naye akimpatia mema ya kimbingu. Uwepo huu wa Mungu ndani mwetu ni utimilifu wa huruma yake kwetu na kwa njia hiyo tunaweza kuuonja upendo wake milele. Ni uthibitisho kwetu wa kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii tukiwa na uhakika wa kuzikabili vilivyo kwa sababu Yeye ambaye anatawala miyoni mwetu ni Mungu na hakuna kinachoweza kushindana naye. Hivyo hapa linadokezwa paji la imani na matumaini kwa kuukubali utawala wake uje na kuwa na hakika ya kupita salama katika taabu zozote pale Yeye anapokuwa ni Mfalme mioyoni mwetu.

Utangulizi huo unahitimisha  kwa kutuambia kwamba “Ufalme wake ni wa haki, mapendo na amani”. Hapa ndipo tunapoweza kuupambanua zaidi ukweli wa Kristo na ule wa dunia hii. Neno haki linamfanya mwanadamu kudai kupata kile anachostahili bila kumjali mwingine. Tuyakumbuke maneno ya mwalifu mmoja pale msalabani: Je, Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi”. Ni kutafuta haki yako kunakorandana kabisa na yanayotendeka katika ulimwengu wa leo. Sheria na taratibu zinawekwa ili kulinda maslahi ya watu fulani hata kama ni kwa kutimbilia mbali haki ya mwingine. Haki ambayo inakosa upendo kwa wengine inapoteza ladha yake. Tunashuhudia leo wenye nacho wanazidi kuneemeka kwa kufuata taratibu zilizopo. Hatuwezi kuwalaumu lakini haki yao hiyo inawafanya kushindwa kumwangalia Lazaro aliye mlangoni kwake.

Mwanadamu katika ulimwengu wa leo anapigana sana kuitafuta haki yake lakini bila kubaki katika ukweli wa msingi. Kila mmoja anao utawala wake kwa kisingizio cha huria ya kimaadili. Hapa ndipo tunapoona jinsi neno ukweli katika ulimwengu huu linavyopoteza nguvu. Kama ni haki yangu kuutoa uhai wa kiumbe tumboni mwangu kwa sababu zangu binafsi tu, je haki ya huyu mwanadamu ninayeumaliza uhai wake ipo wapi? Kama nina haki ya kulipwa mabilioni ya fedha kwa juma sababu ya kucheza mpira, pesa ambazo zinaishia katika anasa na starehe zote za kidunia ipo wapi haki ya mchezaji mwingine ambaye yupo katika dunia ya tatu anayekosa hata lishe bora kwa sababu tu ya ukata na bado ukadiriki kuwashindanisha hao wote katika mashindano yawe ni ya kidunia au ya kikanda? Haki hapa ipo wapi?

Tunapotafuta haki yetu bila kuutazama ukweli tunaupoteza upendo na matokeo yake amani inatoweka katika jamii ya watu. Leo tunaalikwa kusema kama yule mwalifu mwingine pale juu msalabani: “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako”. Mhalifu huyu aliyetubu anatufundisha namna ya kuitafuta haki yetu katika ukweli, yaani kwa njia ya kuukaribisha ufalme wa Kristo mioyoni mwetu. Hapo tu ndipo tutaweza kutoka na kuifanya huruma yake kuenea kwa watu wote. Mwalifu huyu aliyetubu haangaiki kujiangalia yeye. Anapokuwa pale juu msalabani anautambua ukuu wa Mungu, anatambua kwamba hakustahili kufanyiwa ukatili huo, anamtambua kuwa ni Mungu na anaenda mbali zaidi kwa kuonesha huruma kwake akisema “huyu hakutenda lolote lisilofaa”.

Tamko la mhalifu huyu aliyetubu kwamba “huyu hakutenda lolote lisilofaa” ambalo lilimwelekea Yesu ndilo linatuonesha maana ya huruma ya Mungu ambayo inazipita haki zote za kidunia. Ni tamko ambalo linatuonesha nafasi ya upendo katika kuufanya ukweli yaani ile sifa ya ufalme wa Kristo itawale. Ni tamko ambalo linatuonesha namna ya kuitafuta haki yetu katika ukweli na hivyo kutenda kwa mapendo. Kama Kristo angetaka kuitafuta haki yake asingekuwa tayari kuja duniani kwa ajili ya kutukomboa. Mtume Paulo anapomuelezea katika waraka wake kwa Wafilipi kwamba aliiacha namna yake ya kuwa Mungu kusudi aje kumkomboa mwanadamu. Upendo wake unamfanya aiweke rehani haki yake kwa ajili ya kunitafutia mimi binadamu mdhambi haki. Hii ni kwa sababu Yeye ni Mungu na anaongozwa na upendo huo wa kimungu ambao ndiyo unaufanya utawala wa Mungu kuenea duniani kote.

Tunapohitimisha mwaka huu wa huruma ya Mungu tumwendee Kristo kama kabila zote za Israeli zilivyomwendea Daudi zikisema “wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli”. Tumwendee Kristo kusudi ukweli wake uthibitishwe ndani mwetu kwani ni kwa njia ya uwepo wa ukweli huo ndipo haki, mapendo na amani ya Kristo vitadumu ndani mwetu na kutuhakikishia udumifu wa huruma yake.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.