2016-11-18 15:08:00

Kongamano kuhusu: kazi, ugunduzi na uwekezaji!


Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumamosi tarehe 19 Novemba 2016 unaendesha kongamano la kitaifa kwa wajumbe wake kutoka Italia ili kupembua kwa kina na mapana jinsi ya kupambana na ukosefu wa fursa za ajira. Kazi, Ugunduzi na Uwekezaji ni mambo makuu yanayoongoza kongamano hili la siku moja, linalowashirikisha wasomi na wawekezaji kutoka katika sekta zinazotumia teknolojia ya hali ya juu pamoja na waandishi wa habari wa Jarida la “Civiltà Cattolica”.

Mapinduzi ya viwanda ni tema ambayo inaendelea kufanyiwa kazi katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia na wanasiasa, wachumi na wanajamii katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Mageuzi ya viwanda ni changamoto kubwa inayohitaji kupatiwa majibu muafaka kwa kuangalia fursa zilizopo na athari zake katika mfumo mzima wa ajira. Mapinduzi ya teknolojia katika viwanda yanaonekana kuendelea kusababisha ukosefu mkubwa wa fursa za ajira. Kumbe, kuna haja ya kuangalia ni kwa jinsi gani uwekezaji unaweza kuwa ni chanzo cha uchumi shirikishi badala ya kujikita katika uchumi unaobagua watu katika jamii. Vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani wanapaswa kupata fursa za ajira katika mfumo mzima wa mapinduzi ya viwanda duniani!

Mafundisho Jamii ya Kanisa anasema Domingo Sugranyes Bickel, Rais wa Mfuko wa “Centesimu Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema mfumo mzima wa kazi unapaswa kuwa ni fursa ya kuongeza ajira kwa watu sanjari na kuwawezesha watu kuendelea na kujitegemea zaidi; mambo ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la imani kwa masuala ya kazi, ugunduzi na uwekezaji, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi katika kipindi hiki cha digitali.

Mageuzi ya viwanda yanaendelea kusababisha mwelekeo mpya wa maisha unaodhibitiwa na kuratibiwa na mfumo wa mawasiliano ya kijamii kwa njia ya internet, inayowaweka wadau mbali mbali katika mchakato wa uzalishaji wa bidhaa na huduma. Hapa, jambo la kumshukuru Mungu ni kuthamini kipaji cha ugunduzi ambacho kinawajalia watu kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika mchakato wa uzalishaji na utoaji huduma. Lakini jamnbo la kusikitisha ni kuona kwamba, mfumo huu unazalisha idadi kubwa ya watu wasiokuwa na fursa za ajira, matokeo yake, mafao ya wengi hayapewi kipaumbele cha kwanza!

Mfumo wa kazi na ajira unaendelea kubadilika kila kukicha kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika uzalishaji na huduma. Kwa njia ya mawasiliano yaliyoboreshwa kwa kiasi kikubwa, mambo mengi yanafanyika kwa wakati bila kuchelewa, hali inayounda mwelekeo mpya wa mfumo wa kazi duniani unaopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Mfumo mpya wa uzalishaji unapaswa kuwa ni endelevu na unaowashirikisha wengi badala ya kuwatenga na kuwakosesha fursa za ajira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.