2016-11-17 10:13:00

Uinjilishaji mpya unajikita katika ushuhuda na upendo!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na wakuwapongeza wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa huduma na ushuhuda wa upendo wanaoendelea kutoa kwa Makanisa mahalia. Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha, dhamana inayolitaka Kanisa kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia maisha ya kifamilia na kijamii; pamoja na maisha ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu ya binadamu!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 17 Novemba 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza kuu la Wawakilishi wa Caritas Internationalis. Uinjilishaji mpya kwa namna ya pekee unajikita katika ushuhuda na upendo “Confessio et Caritas” kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; ili waweze kushirikishwa katika mustakabali wa maisha yao. Kanisa kwa namna ya pekee, linapaswa kusimama kidete kupinga utamaduni wa ubaguzi na kutowajali wengine katika shida na mahangaiko yao na badala yake, watu wajizatiti katika ujenzi wa sanaa ya mshikamano ili wenye nguvu waweze kuuchukua udhaifu wa wanyonge bila kujipendelea wenyewe.

Baba Mtakatifu anasema, maneno haya ni msingi wa utume na maisha ya Kanisa yanayotekelezwa kwa njia ya Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kitaifa na Kimataifa kwani ni sehemu ya utume wa Kanisa na wala si wakala wa misaada. Ni Mashirika ambayo yanapaswa kushikamana bega kwa bega na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia ili kuwasaidia kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao upendo kwa familia ya Mungu, kwa kuwa na kipaji cha ugunduzi katika upendo, ili kutekeleza dhamana hii kwa ufanisi kwa kuwa jirani na wasamaria wema, ili kushirikiana na kidugu na wale wanaoteseka na kuelemewa na mizigo ya maisha. Lengo ni kuhakikisha kwamba, upendo na haki katika mwanga wa Injili pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa vinang’ara, kwa kuwashirikisha maskini wenyewe ili waweze kuwa ni wadau wa mustakabali wa maendeleo yao.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kwa niaba ya Mama Kanisa kuwashukuru kutokana na majitoleo yao kwa maskini na kuwataka kuendelea na utume huu, ili kuwawezesha watu kujisikia kwamba, Kanisa ni chombo cha matumaini yanayowasindikiza watu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Caritas Internationalis iendelee kutangaza Injili ya furaha ili kuwasaidia wale waliobaki nyuma pamoja na kuwajengea uwezo wale wenye fursa za kuleta mageuzi katika maisha. Inawezekana kabisa kuupatia umaskini, njaa, magonjwa na dhuluma kisogo kwa kujiaminisha kwenye nguvu ya Injili inayoweza kubadili au kuboresha hali ya maisha ya watu. Ni wajibu wa Kanisa kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu wa wale wanaosubiri alama ya upendo; kulinda na kujenga nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anaitaka Caritas Internationalis kuwa na ujasiri wa kinabii kwa kukataa katu katu mambo yote yale yanayomdhalilisha na kumnyonya binadamu; kwa kujenga mihimili ya upendo na mshikamano kwa ajili ya kuangazia maisha ya watoto na wazee; wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta amani ya kweli. Baba Mtakatifu anaishukuru Caritas Internationalis ambayo imeamua kujitwika mzigo wa kampeni kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kuonja ukarimu na upendo kutoka kwa Wasamaria wema na hivyo kujisikia nyumbani kwenye Jumuiya zinazowahifadhi. Ni dhamana na wajibu wa Caritas kuendeleza mchakato wa maendeleo na amani katika maeneo ambamo watu wanakimbia vita au wanataka maisha bora zaidi.

Caritas Internationalis inapaswa kuwa ni wajenzi na wasaniii wa: haki, amani na upatanisho kwa kushirikiana na wadau wengine katika imani, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu wa binadamu. Wasimame kidete kupambana na umaskini na kuendelea kujifunza kutoka kwa maskini katika hali yao ya unyenyekevu na kiasi; tunu msingi za maisha yao; mshikamano na umoja. Wajifunze jitihada zao za kupambana na umaskini kwa kuangalia imani yao inayobubujika kutoka katika mateso ya Kristo Yesu, Bwana na Mkombozi. Wajifunze maisha yao ya sala, imani na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu.

Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, ni matumaini yake kwamba, Caritas Internationalis wataendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utume wa upendo, kwa kuwasaidia waamini kuwa ni majukwaa ya ushuhuda na Uinjilishaji wa Habari Njema ya Wokovu; kwa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na huduma kwa maskini katika hali ya furaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.