2016-11-17 07:43:00

Pale ndoto ya Upadre inapofutika?


Askofu mkuu Antonio Giuseppe Calazzo wa Jimbo kuu la Mater-Irsina, Italia, Ijumaa tarehe 18 Novemba, 2016 anatarajiwa kutoa Daraja ya ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi wawili kutoka Tanzania nao ni: Nicas Francis Shirima na Wilhard Casmir Shayo wa Shirika la Mapendo, maarufu kama “Rosminians”. Ibada hii ya Misa itafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane, Porta Latina, Roma.

Ifuatayo ni historia fupi ya Shemasi mteule Shayo! Naitwa Wilhad Casmir Shayo ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto saba (Wanne ni wa kiume na watatu ni wakike). Nilizaliwa tarehe 6/8/1980 Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Nlijiunga na shule ya Msingi Maretadu Juu Mkoani Arusha (Kwa sasa Mkoa wa Manyara) mwaka 1989 na baada ya baba kupata uhamisho kwenda Moshi mwaka 1992 niliendelea na masomo yangu katika Shule ya Msingi Mrawi iliyopo wilaya ya Moshi Vijijini.

Nilivutiwa na maisha ya kumtumikia Mungu kama Padri tangu nikiwa na miaka minane. Hii ni kutokana na msingi mzuri wa sala niliopewa na wazazi wangu pamoja na babu yangu. Nikiwa mdogo nilivutiwa kuona watoto wengine wenye umri kama wangu wakitumikia misa nami nilipenda sana kutumikia. Nilijiunga na Shirika la Mtakatifu Aloisi ambapo pamoja na maisha ya sala kama kikundi cha vijana, tulihusika katika kutumikia misa pia. Nilivutiwa kujiunga na Seminari baada ya Elimu ya Msingi lakini kutokana na kukosa nafasi nilijiunga na Shule ya Sekondari Mnini mwaka 1996-1999 nilipohitimu kidato cha nne.

Niliomba kujiunga na Shirika la Wasalesiani wa Yohane Bosco. Matokeo ya kidato cha nne yalipotoka yalionyesha nimefaulu kwa kupata daraja la kwanza. Nilipangwa kusoma Shule Ya Ufundi Tanga kwa mchepuo wa Sayansi (Physics, Chemistry na Mathematics). Kutokana na hali ya kiuchumi kuwa si nzuri sikuweza kujiunga na Shirika la Yohane Bosco badala yake nilijiunga na Tanga Technical Secondary School mwaka 2000-2002.

Nikiwa shuleni hapa wazo la kujiunga na Maisha ya kumtumikia Mungu lilipotea miezi ya mwanzo nikiwa kidato cha tano. Pamoja na hayo niliendelea kusali na wenzangu wakati wa vipindi vya dini pamoja na mikusanyiko ya sala kwa Vijana Wakatoliki Tanzania (T.Y.C.S). Mnamo  mwezi Oktoba mwaka 2000 nilichaguliwa kama Mwenyekiti wa Tawi na mwaka uliofuata kama Mwenyekiti wa TYCS Jimbo la Tanga.

Nikiwa kidato cha tano mwezi Novemba nilipokea barua ya mwaliko kutoka kwa Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Mapendo kwa mwito wa Workshop. Mimi pamoja na wenzangu wanne (Anold Matto, Alfons Bikulamuchi, Nestor Mosha na Emanuel Hamaro) tuliungana na wenzetu kutoka Shule za Sekondari Galanos na Usagara kwa ajili ya mkutano huu. Tulikutana na Wakurugenzi wa miito wa mashirika matatu: Wayesuit, Wadominican pamoja na Shirika la Mapendo. Ni kupitia mkutano huu, ndoto niliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu katika maisha yangu ilirejea kwa nguvu zaidi.

Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2002 niliomba kufundisha katika Shule ya Sekondari Sangiti iliyokuwa ikiongozwa na Masista wa Shirika la Assumption kuanzia Mwezi July 2002 hadi Septemba 2003.Kuwapo shuleni hapa, nileiendelea kupata msukumo mkubwa wa kujiunga na maisha ya Upadre kutokana na ushauri niliopata kwa masista hawa ambao walinialika kusali pamoja na kujumuika katika Ibada ya misa Takatifu pamoja nao. Nakumbuka Sista Honorata na Sr. Catherini kwa nyakati tofauti wakiniambia kuwa wanafikiri Mungu anapenda nimtumikie. Walikuwa wakiniombea na kunishauri mara kwa mara. Ni wakati huu ambapo niliwajulisha wazazi wangu dhamira ya kujiunga na maisha ya Kumtumikia Mungu. Walinishauri kufanya tafakari juu ya uamuzi huu ikiwemo kusali. Mara baada ya kufanya hivyo niliwaeleza kwamba nimeridhia kujiunga na maisha hayo na walinipa baraka zao. Mnamo tarehe 15/09/2003 nilijiunga na Shirika la Mapendo nikiwa mmoja kati ya wenzangu kumi.

Tarehe 17/06/2006 niliweka nadhiri za mwanzo katika nyumba yetu ya Novisiati huko Lushoto, Tanga na nilitumwa Nairobi, Kenya kusomea Shahada ya Elimu katika Sayansi katika masomo ya Fisikia na Kemia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (C.U.E.A).Nilianza masomo mwezi Agosti mwaka 2007-2010. Mara baada ya kuhitimu masomo yangu nilijiunga na Chuo cha Tangaza kwa mwaka mmoja (2010-2011) Kusomea Cheti katika masomo yahusuyo Utume kwa vijana. Baada ya kumaliza masomo haya, nilitumwa kufundisha pamoja na kuwa Msaidizi wa  Mkuu wa Shule ya Rosmini Sekondari huko Tanga. Nilidumu shuleni hapa kwa muda wa miaka miwili (2011-2013). Tarehe 12/01/2013 nilifanya nadhiri za daima. Tarehe 11/09/2013 nilitumwa Roma Italia kuja kusoma masomo ya Falsafa/Taalimungu katika Chuo cha Kipapa Cha Mtakatifu Beda.

Katika masomo yangu nilijifunza mengi kuhusu Maisha ya sala pamoja na uhusiano wangu na Mungu pamoja na binadamu. Nilijifunza mengu kuhusiana na mwanzilishi wa Shirika letu Mwenyeheri Antoni Rosmini hususan Kanuni ya maisha ya Utakatifu. Masomo haya pamoja na maisha ya Jumuiya vimenifundisha na kunipa mwanga wa ukuu wa Mungu kwetu sisi kama binadamu. Katika maisha yangu ya sala nimekuwa nikimwomba anisaidie na aniongoze ili siku moja nimtumikie katika kanisa lake.  Nimekuwa nikiwaombea vijana kama mimi pia waweze kuguswa na nguvu ya Roho Mtakatifu ili watolee maisha yao katika kumtumikia Mungu.

Natarajia kutimiza sehemu ya  Ndoto yangu mnamo tarehe 18/11/2016 siku ambayo nitapewa daraja ya Ushemasi wa mpito! Nawashukuru wazazi wangu, wadogo zangu, babu na bibi(Mungu awape pumziko la milele), waalimu, walezi katika shirika, ndugu wengine katika ukoo wetu, wote walionisaidia na kuniombea pamoja na wanashirika la mapendo kwa misaada yao mbalimbali ikiwepo kuniombea katika kutimiza ndoto hii. Mungu awabariki na kuwajalia hamu ya mioyo yao.

Frateri Wilhad Shayo.








All the contents on this site are copyrighted ©.