2016-11-17 16:34:00

Kilio cha Mungu kwa binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Siku ya Alhamisi, tarehe 17 Novemba 2016 anasema, Injili ya Siku inamwonesha Yesu aneyelilia Hekalu la Yerusalemu kwa kukumbuka historia ya watu wake, walionjeshwa upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, lakini kwa bahati mbaya wakaendelea kuwa watu wenye shingo ngumu, waliokosa uaminifu na hatimaye wakawa ni watenda dhambi wakuu. Hata katika hali na mazingira kama haya Mwenyezi Mungu bado aliendelea kuwa na upendo usiokuwa na kifani kwa watu wake.

Kuna Manabii kama Hosea na Yeremia walioonesha na kushuhudia upendo mkubwa kwa Mwenyezi Mungu na Israeli, lakini watu walishindwa kuona na kuonja upendo huu, pale Mwenyezi Mungu alipowatembelea watu wake! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu alisikitishwa sana na ukaidi pamoja na ukosefu wa uaminifu ulioneshwa na watu wake, kiasi cha kushindwa kuonja huruma na upendo wa Mungu kati yao; Mungu ambaye daima alijitaabisha kuwapenda na kuwatafuta, ili kuwakirimia furaha na amani ya ndani. Yesu alisikitika moyoni mwake, kwa kutambua hatima ya maisha yake kwa mateso, kifo na ufufuko wake, mchakato wa maisha endelevu ya Yesu hata nyakati hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kila mwamini anapaswa kujiuliza moyoni mwake, ikiwa kama aliweza kutambua uwepo wa Mungu katika historia na maisha yake, pale alipomtembelea ili kumwonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Pale alipobisha hodi kwenye malango ya mioyo yao, lakini wakashindwa kumfungulia, tofauti na Zakayo Mtoza ushuru aliyejitambua kuwa ni mdhambi na mfupi wa kimo, akawa tayari kujitaabisha kutafuta fursa ya kukutana na Uso wa huruma ya Mungu, akatubu na kumwongokea Mungu; akawa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wale aliokuwa amewatenda vibaya.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kuwa, kila mwamini anaweza kujikuta ametumbukia katika dhambi kama waliyotenda Waisraeli na Yerusalemu kwa kushindwa kutambua nyakati walipotembelewa na Mungu. Lakini waamini wakumbuke kwamba, kila siku ya maisha yao, Yesu anaendelea kubisha hodi kwenye malango ya mioyo yao, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanaitambua na kuijibu sauti ya Kristo inayoendelea kubisha hodi. Waamini wasijiridhishe kwa kuwa na usalama wa mambo mpito na kwa kuhudhuria Ibada kila siku; lakini jambo la msingi ni kuchunguza dhamiri, ikiwa kama wamegundua kwamba, Mwenyezi Mungu amewatembelea, ili kugeuza uwepo wake katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Waamini wanapotembelewa na Yesu ili kuwamegea upendo wake usiokuwa na mipaka, wasiogope kumkaribisha kama anavyoonya Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa! Waamini wawe na ujasiri wa kumtambua kwani anawakirimia neema na baraka za kuweza kugundua na kuonja uwepo wake katika maisha yao. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua na kuonja uwepo wa Mungu anapowatembelea katika historia na hija ya maisha yao ya kila siku, ili kweli nyoyo yao, iweze kuzama na kuogelea kwenye upendo wa Mungu, tayari kuwashirikisha wengine, pendo hilo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahii ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.