2016-11-17 07:19:00

Huruma na upendo wa Mungu unaendelea kuwaambata watu wake!


Kufuatia machafuko ya miezi ya hivi karibuni katika Jamhuri ya Afrika ya kati, linaibuka swali la msingi kujiuliza: iwapo tukio la Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchi hiyo mwaka jana 2015, limepoteza matunda ya miujiza iliyosemekana kutendeka katika taifa hilo! Jibu linaonekana kuwa moja na sahihi kwamba: mbegu iliyopandwa na Baba Mtakatifu Francisko katika safari yake hiyo haikuanguka kwenye mwamba bali kwenye udongo mzuri, na matunda yake yanaonekana kwenye uongofu na uhuru wa ndani wa watu wengi katika taifa hilo. Inaeleweka pia kwamba, kawaida Mungu habidili historia kwa kutumia wenye nguvu, bali anatumia wanyonge, wenye kuonewa, wanyenyekevu, wale wachache wanaovumilia mateso mpaka mwisho.

Hii ni sehemu ya mahubiri ya Kardinali mteule Dieudonné Nzapalainga, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, alipokuwa akiadhimisha Misa Takatifu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, jumapili iliyopita 13 Novemba 2016. Amewaasa waamini kudumu katika hija msingi ya wokovu na uhuru inayopatikana katika huruma ya Mungu, na kwamba wadumu katika matumaini sababu Mungu hajawasahau, anasikiliza sala zao walio wanyonge na ataibua jua la haki liwaangazie walio wateule wake.

Kardinali mteule Nzapalainga kaadhimisha Misa ya kufunga Mlango Mtakatifu wa Huruma ya Mungu katika Kanisa kuu la Bangui, mlango uliofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko mwaka jana 2015, tarehe 29 Novemba, alipoitembelea nchi hiyo. Baadhi ya maaskofu, mapadri na umati mkubwa wa waamini kutoka pande zote za Jamhuri ya Afrika ya kati, wamependa kufanya tena hija ya kupita katika mlango huo mtakatifu wa Huruma ya Mungu katika Kanisa kuu la Bangui. Ishara ya hija hiyo, ni ya kudumu katika kujifunza na kuishi Huruma ya Mungu, hija ambayo ni ndefu bado kwa mwanadamu. Katika kuwakumbusha maneno ya msingi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyowaasa mwaka jana, Kardinali mteule Nzapalainga kawasisitiza kutilia maanani ujumbe mzito aliousema Baba Mtakatifu kwamba: Bangui umekuwa mji mkuu wa kiroho kwa dunia nzima.

Inawezekanaje kufikiria taifa la kesho wakati watu wanaendelea kuuwawa, kunyanyaswa, vitu kuchomwa, watu wanakimbia nchi yao, watoto hawaendi shule katika sehemu kubwa ya taifa, wafanyakazi wanaogopa kufika sehemu za kazi walizopangiwa, kukosekana kwa huduma za afya! Kardinali mteule Nzapalainga, anawaalika kila mmoja kutafakari na kujijibu wajibu wake na nafasi yake ya kutatua mahangaiko na changamoto hizo. Misa hiyo ikiwa imehudhuriwa na mke wa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya kati, Waziri mkuu, Spika msaidizi wa bunge, na mawaziri kemkem, Kardinali mteule Nzapalainga amewaalika kila mmoja kuacha tabia za kukwepa majukumu na kutupiana lawama, wakati damu ya watu wasio na hatia inazidi kumwagika, badala yake wachukue hatua ili amani irudi nchini humo.

Pamoja na ukweli kwamba wapo wenye kutenda maovu na kuharibu amani ndani ya nchi hiyo, kuna wengi waliobaki waaminifu, wanaotenda mema na kuendelea kuliombea taifa lao, amesema Kardinali mteule Nzapalainga, huku akitahadharisha kwamba, atendaye maovu hataurithi Ufalme wa mbinguni. Amemwalika kila mmoja kuitikia wito wa Mungu kuwa vyombo vya amani. Akitolea mfano, kawapongeza wana harakati wote wa kutafuta amani na haki nchini humo, wakiwemo ma Imam na wazee wa hekima wa Km5, wanaowashawishi vijana kutupa silaha na kutafuta njia za mazungumzano zaidi. Huu ni mwaliko kwa wote, wawe wakatoliki, waprotestanti, au waislamu. Baadhi ya matunda yameonekana tena, kwani siku iliyofuata baada ya mahubiri hayo, wameachiliwa huru wafungwa wawili wa kisiasa nchini humo.

Askofu mkuu Dieudonné Nzapalainga atasimikwa rasmi hapo tarehe 19 Novemba 2016, katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican na wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme wa ulimwengu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Makardinali wote wapya, ili kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, hija ambayo sasa inapaswa kuwa endelevu katika maisha ya waamini: kiroho na kimwili!

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.