2016-11-16 14:52:00

Vatican kushiriki Onesho la Expo Astana 2017


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwa niaba ya Vatican, kunako tarehe 29 Aprili 2016, aliweka sahihi ya kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa nchini Kazakhstan, tayakayoanza kutimua vumbi hapo tarehe 10 Juni hadi 10 Septemba 2017. Tayari kamati ya maandalizi ya ushiriki wa Vatican katika tukio hili la kimataifa imekwisha kutembelea mjini Astana na kukutana na viongozi wa Kanisa mahalia, watakaoshirikiana kwa karibu zaidi katika onesho hili. Wachunguzi wa mambo wanasema, hii ni changamoto kubwa na fursa ya pekee kwa Kanisa lenye idadi ndogo ya waamini kuweza kushiriki katika tukio hili la kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, Vatican imekuwa ni mshiriki mkuu wa Maonesho mbali mbali ya kimataifa, ili kuchangia kwa kina na mapana Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu tema mbali mbali kama vile: Maji kama haki msingi ya binadamu; Onesho lililofanyika huko Zaragosa kunako mwaka 2008; Chakula, Onesho la EXPO Milano kwa mwaka 2015 na sasa Vatican inajiandaa kushiriki katika onesho la Expo Astana 2017. Kama sehemu ya maandalizi ya Onesho hili kumeandaliwa tema itakayowasilishwa na Vatican kwenye onesho hili kwa kuwa na mambo msingi ambayo Vatican inapenda kuyaonesha.

Tarehe 16 Novemba 2016, Kardinali Peter Turkson pamoja na viongozi wa Kanisa mahalia kutoka Kazakhstan wamewasilisha tema itakaongoza Onesho la Expo Astana 2017 kwa waandishi wa habari. Tema hii inaongozwa na kauli mbiu “Nishati kwa mafao ya wengi: kulinda mazingira nyumba ya wote”. Ni muhimu kuwasilisha hati hi inchini Kazakistan, mwenyeji wa Onesho la Expo Astana 2017, nchi ambayo imebahatika kuwa na uwepo wa waamini wa dini, imani na mapokeo mbali mbali, mambo yanayounda na kujenga utajiri wa mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene.

Nishati rafiki kwa mazingira ni kati ya changamoto kubwa zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa nyakati hizi, kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kujenga utamaduni wa uwajibikaji unaojikita katika usawa na ushirikishaji wa wengi kwa ajili ya maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Tema hizi ni muhimu sana na zimechotwa kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama yalivyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume “Upendo katika ukweli” “Caritas in veritate” wa mwaka 2009 “Sifa iwe kwako; juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” “Laudato si” uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2016 sanjari na tafakari ya kina inayofanywa na wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira huko Marrakech, Morocco, COP22. Baraza la Kipapa la haki na amani kunako mwaka 2013 liliandaa tema kuhusu: nishati, haki na amani, kitabu ambacho kwa sasa kinapatikana katika lugha mbali mbali za kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.