2016-11-16 15:13:00

Papa Francisko atuma kikosi kazi Norcia kusaidia kazi ya uokoaji!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuguswa na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu pamoja na nyumba za Ibada kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba Italia hivi karibuni, ametuma kikosi kazi cha wataalam kutoka katika kitengo cha makumbusho ya Vatican kinachojishughulisha na ukarabati wa sanaa za Kanisa pamoja na wanajeshi wa Kikosi cha zimamoto kwenda kwenye eneo lililoharibika zaidi, Jimbo  kuu la Spoleto-Norcia. Kikosi kazi hiki kinaongozwa na Mhandisi Paolo De Angelis na kinashirikiana na Kikosi cha zimamoto cha Serikali ya Italia, ili kuokoa sanaa za Kanisa ambazo zmeharibiwa kwa kiasi kikubwa na tetemeko la ardhi pamoja na kuwasaidia wananchi kuokoa sehemu ya mali zao.

Askofu mkuu Renato Boccardo amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa karibu kwa wananchi waliokumbwa na tetemeko la ardhi. Wengi bado wanamkumbuka alipowatembelea huko Norcia, tarehe 4 Oktoba 2016 pamoja na simu aliyomtwangia Askofu mkuu Boccardo akimwomba amfikishie salam na matashi kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na majanga asilia. Kikosi kazi hiki kutoka kwa Baba Mtakatifu, kitafanya kazi hii ya kujitolea kama kielelezo cha upendo na mshikamano kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro anayeguswa na mahangaiko ya watu wake: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.