2016-11-15 15:17:00

Mh. Pd. Dominique Banlène Guigbile ateuliwa kuwa Askofu


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Jacques Nymbusède Tukumbè Anyilunda wa Jimbo Katoliki Dapaong, Togo na wakati huo huo, amemteua Mheshimiwa Padre Dominique Banlène Guigbile, kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Dapaong. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Makamu Askofu katika kuratibu shughuli za kichungaji.

Askofu mteule Dominique Banlène Guibile alizaliwa kunako tarehe 30 Desemba 1962 Jimboni Dapaong. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 30 Desemba 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya hapo amekuwa ni Paroko usu, Mkurugenzi wa kituo cha semina cha Jimb. Kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2002 alikuwa nchini Ufaransa kwa masomo ya juu. Kuanzia mwaka 200-2 hadi mwaka 2009 alikuwa ni Paroko na Katibu mkuu wa Umoja wa Mapadre wa Majimbo nchini Togo.

Kuanzia mwaka 2003 akateuliwa kuwa ni Makamu Askofu na mratibu wa shughuli za kichungaji kijimbo. Mwaka 2009 akateuliwa kuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro huko Korbongou. Askofu mteule ni mjumbe wa Baraza la Wakleri Jimbo, Msahauri wa Askofu na mjumbe wa Kamati ya uchumi na maendeleo ya Jimbo pamoja na kuwa ni Jaalim wa Seminari kuu ya Falsafa na Taalimungu Togo pamoja na Chuo kikuu cha Serikali cha Kara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.