2016-11-15 15:01:00

Iweni chachu ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa pia ni fursa kwa waamini kufanya hija inayowakumbusha kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makao ya kudumu. Ili kuweza kulifikia Lango la huruma ya Mungu kuna haja ya kuwa na majitoleo pamoja na kufanya sadaka, kama chemchemi ya wongofu wa ndani; kwa kushikamana na kuiambata huruma ya Mungu, tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wake!

Mahujaji kutoka katika Nchi za Scandinavia, Jumanne, tarehe 15 Novemba, 2016 wameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye kusalimiwa na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Siku ya Jubilei ya familia ya Mungu kutoka Holland, kielelezo cha umoja wa Kanisa katika Nchi za Scandinavia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mwaka wa huruma ya Mungu umewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele, ushuhuda wa Fumbo la upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Hii ni chemchemi ya uzima wa milele. Watu wote wanahitaji kuonja na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani anaokoa, anawajalia maisha mapya na kupyaisha maisha yao, ili waweze kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wanaonja wema wa ukombozi wa Mungu. Sakramenti ya Upatanisho ni mahali ambapo waamini wanapokea zawadi ya msamaha na huruma ya Mungu na huo unakuwa ni mwanzo wa mabadiliko katika maisha ya waamini na chachu ya mabadiliko pia katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufungua nyoyo zao ili ziweze kupambwa na huruma ya Mungu, ili wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, tayari kuwashirikisha wengine, msamaha na kushuhudia wema na upendo wa Mungu kwa waja wake. Walimwengu wana njaa na kiu ya kutaka kuonja wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Kumbe, waamini hawa wanaweza kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuzima kiu ya watu hawa sanjari na kuwasaidia watu kumgundua Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Kama mitume na wamissionari wa Yesu wanaweza kumwagilia jamii kwa kutangaza na kushuhudia Injili inayojikita katika upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.