2016-11-15 15:32:00

Adui wa habari zaidi huko Mashariki ya Kati ni Ujinga!


Kila kilima cha ibada ya sanamu kwa mwanadamu, biashara, faida inayotafutwa hata kwa kumwaga damu, vinafaa kushindwa na kugeuzwa kwa kufungua njia za kurudi nyumbani, kujenga utamaduni wa kukutana kati ya watu, ili kuadhimisha Ibada ya kweli na ya rohoni. Ndugu msikilizaji sikia maneno mazito hayo na ya kuvuvia roho, ambayo Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, ameyatumia Jumapili iliyopita, tarehe 13 Novemba 2016, katika kumalizia hotuba yake ya kufunga kongamano la Damasko mche wa matumaini. Kongamano lililoandaliawa na Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki iliyo Roma, katika kukumbuka miaka 100 ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Lengo la Kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu, tangu tarehe 11 – 13 Novemba, ni kutoa fursa ya kukutana na kuzungumza, na zaidi sana kutoa mwanga kwa hali halisi ya Makanisa ya Mashariki ya kati, yenye matukio mengi ya kusisimua. Kardinali Sandri amekumbushia maneno ya Askofu mkuu wa Orthodox-siria, Yohana Ibrahim aliyetekwa mwaka 2013 pamoja na mtawa wa kiume wa Orthodox-ugiriki, Boulos Yazigi, Kardinali Sandri anatumia maneno ya Askofu mkuu Yohana Ibrahim kutahadharisha kwamba: adui wa hatari zaidi ambaye Wakristo na Waislamu wanapaswa kumkabili ni ujinga. Ujinga ambao ndio unatawala wakati wa mazungumzano ya kidini, kiasi cha kuleta hofu na vurugu kati ya wakristu na waislamu.

Hata hivyo, ujinga huo unaweza kushindwa katika vituo vya elimu kama ambavyo Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki inavyofanya. Hilo wanaweza kulishuhudia waseminari, mapadri, watawa wa kike na wa kiume wanaokutana katika taasisi hiyo, wakijitambua kuwa wanatoka sehemu tofauti tofauti za Makanisa ya Mashariki ya kati, bado wanafanya hija ya pamoja kuelekea kisima cha ufahamu wa taalimungu, maisha ya kiroho na liturjia, vilivyo utajiri wa tamaduni za makanisa ya mashariki ya kati, wakitafuta umoja wa wakristu wote.

Haitakuwa rahisi, anasema Kardinali Sandri, kwani wanafahamu pia kwamba kwa hali kama ya Siria na Iraq, kuna matamko ya umwagaji damu kwa wafuasi wa Kristu, na hata wale wasio wakristu. Haya yanatendwa na baadhi ya watu wa itikadi kali na nadharia zisizovumilia maisha ya pamoja kwa watu wa mitazamo na itikadi tofauti. Inaonekana wana lengo la kufutilia mbali kumbukumbu ya mema, maisha ya amani ya pamoja, ya utendaji wa sanaa na uandishi, na siasa safi.

Pamoja na hayo, hata siku moja uovu hawezi kuwa ndio neno la mwisho, uovu hauwezi kutawala, amesisitiza Kardinali Sandri. Kwa sababu hiyo, Kanisa litaendelea kuhangaika ili watoto na vijana wa Siria na Iraq wapate kurudishiwa mwanga wa matumaini kwa siku za usoni, tumaini la maisha ya amani na upendo katika nchi zao, na kwa wakazi wake. Baba Mtakatfu Francisko, anapenda kutumia maneno haya ya nabii Yoeli, kwamba: waamini wanapaswa kuwa kama wazee wenye ndoto za kuwasaidia vijana kuona maono ya maisha bora ya siku za usoni. Hii inapaswa kuwa nia ya kila mmoja kwa ajili ya mema ya watu wa mashariki ya kati.

Patriaki wa  Antiokia ya madhehebu ya Ugiriki-Melkiti, Askofu Gregorios III Laham amesema kwamba: matumaini yapo makubwa ya amani kurejea tena maeneo ya Mashariki ya kati. Iwapo kutoka barabara za Damasko Injili na amani ilihubiriwa kwa duinia nzima katika karne za kwanza, inawezekana kabisa kwa karne hii, amani toka sehemu zingine duniani ikahubiriwa Siria na maeneo ya Mashariki ya kati, kupitia barabara hizo hizo za Damasko.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.