2016-11-14 12:08:00

Wanamichezo wanaweza kuchangia ujenzi wa jamii ya haki na mshikamano


Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Mabingwa wa mpira wa miguu duniani kutoka katika Timu ya Taifa ya Ujerumani, waliomtembelea mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 14 Novemba 2016. Amewashukuru na kuwapongeza kwa kucheza katika hali ya ushirikiano kama timu moja hali ambayo imewawezesha kutwaa ubingwa katika mashindano mbali mbali. Michezo hasa Mpira wa miguu anasema Baba Mtakatifu, unahitaji nidhamu, sadaka pamoja na heshima kwa wanamichezo wengine bila kuwasahau wanamichezo wa timu husika.

Changamoto hii inawafanya wanamichezo kujenga na kudumisha uwajibikaji hata nje ya viwanja vya michezo, hususan miongoni mwa vijana ambao mara nyingi wanawaona kuwa kama ni mifano bora ya kuigwa. Ni nafasi inayowawezesha hata kushiriki katika masuala mengine ya kijamii kama kielelezo cha mshikamano  na mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu anawashukuru wachezaji wa Timu ya Taifa ya Ujerumani kwa kuchangia kwa hali na mali kwenye miradi inayoendeshwa na “Utoto Mtakatifu” nchini Ujerumani, maarufu kama “Sternsinger” kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenzao wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani. Kwa njia hii, inawezekana kabisa kuvuka kuta zinazowaathiri maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kushiriki katika ujenzi wa mchakato wa jamii inayojikita katika haki na mashikamano! Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kumtembelea na amewatakia heri na baraka katika masuala ya michezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.