2016-11-14 11:36:00

Lango la huruma ya Mungu litaendelea kuwa wazi daima!


Huruma  na upendo wa Mungu vyadumu milele! Kwa kufunga Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, waamini wanafungua lango la maisha yao ya kiroho ili kuanza safari ya maisha ya kiroho katika imani, matumaini na upendo. Lango la huruma ya Mungu wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu limefungua mlango wa maisha ya kiroho ambao ni Kristo Yesu, amani ya watu wake; kiungo cha umoja unaobomoa kuta za utengano na uadui.

Mlango ulio wazi ni kielelezo cha Fumbo la Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa huduma na mapendo na kwamba, huruma yake yadumu milele kama anavyoimba Mzaburi. Waamini wanahitaji nyakati kama hizi ili kuweza kupyaisha, kuimarisha na kuidumisha imani. Mwaka wa huruma ya Mungu kilikuwa ni kipindi kizito cha imani kinachofikia sasa kilele chake kwa kufunga Makanisa makuu pamoja na Madhabahu ya huruma ya Mungu, waamini wakiwa wametakasika. Lakini, ikumbukwe kwamba, Lango la huruma ya Mungu litaendelea kubaki wazi!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali James Michael Harvey, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya kufunga Lango la huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma, Jumapili tarehe 13 Novemba 2016 wakati wa Masifu ya Jioni. Kanisa hili limekuwa ni kati ya Makanisa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yalitengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika wongofu wa ndani na msamaha.

Limekuwa ni Kanisa la maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo yaliyotangazwa na kuzinduliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II; Mwaka 2008 – 2009 Mwaka wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, Kanisa likakumbuka Jubilei ya miaka 2000 tangu kuzaliwa kwake. Haya ni maadhimisho yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Familia ya Mungu ilipata nafasi ya kutafakari Nyaraka mbali mbali zilizoandikwa na Mtume Paulo; nyaraka ambazo zinaunda nusu ya Kitabu cha Agano Jipya.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu amepitia Lango la huruma ya Mungu, ili kusali na kuomba neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu. Ikumbukwe kwamba, lango la huruma ya Mungu kamwe daima liko wazi, ili kuwaunda waamini waweze kufanana na Kristo Yesu, ufunuo wa huruma ya Mungu.

Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma, limeshuhudia idadi kubwa ya waamini na watu wenye mapenzi mema waliofika mahali hapa patakatifu ili kutafakari Neno la Mungu; kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, ili kupata uponyaji wa ndani. Pengine, Kanisa halina takwimu maalum kuhusiana na watu walioguswa na kuponywa na huruma ya Mungu, lakni, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha ujasiri wa kitume kwa kuitisha na kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na waamini wakaonesha mwitikio wa hali ya juu kabisa. Familia ya Mungu imepata nafasi ya kutafakari Uso wa huruma ya Mungu kwa mwaka mzima, changamoto ni kuendelea kuzamishwa katika bahari ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.