2016-11-14 07:26:00

Kanisa ni shuhuda na chombo cha amani duniani!


Ni lazima kufanya juhudi ya kutosha ya utafiti ili kumuelewa vema Baba Mtakatifu Bededikto XV, aliyeliongoza Kanisa katika kipindi cha vita ya kwanza ya dunia. Baba Mtakatifu huyu, tangu Barua yake ya kitume Ad beatissimi, yaani Kwa wenye heri, ya Novemba 1914, alidhihirisha wazi nia yake ya kutojihusisha na watawala wa kidunia. Uchaguzi ambao ulipelekea upingaji na mashambulizi dhidi ya Kanisa na watumishi wake wakleri. Kwa utangulizi huo, ndivyo Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, anavyoanza kuwasilisha mada yake mjini Bologna, Italia, katika Warsha ya historia juu ya Benedikto XV, tangu tarehe 3 – 5 Novemba, 2016.

Uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto XV unatokana na uhalisia wa historia ya karne ya ishirini, historia ya kilichosemekana kuwa vita takatifu au uhasi dini wa kisasa. Kwa namna hii, Baba Mtakatifu huyu alijaribu kutafuta uwiano wa kuendelea kuheshimu mamlaka za dunia kama afundishavyo Mtume Paulo (Rej., Warumi 13, 1), na ile kanuni  ya siku za mwisho, kuhusu amani kama nyenzo ya utangazaji Injili ya Ufalme wa Mungu. Lengo lake kuu, lilikuwa kubadili mtazamo wa tawala za enzi hizo za kutafuta mambo kwa nguvu, badala yake kujenga utamaduni wa Kanisa unaojali zaidi dawa ya msamaha.

Baba Mtakatifu huyu ndiye aliyekamilisha kazi ya kuandika gombwe la kwanza la sheria za Kanisa, 1917, sheria ambazo zilianza kulenga zaidi kama nyenzo ya jumuiya ya kikristo na nyenzo ya wokovu wa watu. Ndiyo sababu alishutumu vita kwa kuiita mauaji yasiyo na manufaa. Ulaya ya kipindi hicho, ilijikuta ikiangukia kwenye dimbwi kubwa la umwagaji damu kwa vita, sababu ya kuhadaika na nadharia ya Sigmund Freud, kuchanganya maisha na machafuko.

Umuhimu wa kumfanyia utafiti wa kina na kumfahamu Baba Mtakatifu Benedikto XV, unakuja sababu ya kitendawili kigumu cha utawala wake na diplomasia yake, wakati wa mitazamo hasi dhidi ya uhai na dhidi ya wakleri. Pamoja na tafiti nyingi zilizofanyika juu ya vita ya pili ya dunia, Baba huyu alibaki kutofahamika sana kwa jitihada zake na namna yake, wakati wa vita ile ya kwanza ya dunia. Ferdinand Hayward mnamo 1955, ndiye aliyefungua macho ya wengi kwa kuandika historia fupi ya Papa huyu.

Monsinyo Antonio Scottà katika vitabu vyake vilivyochapishwa 2002 na 2009, amefafanua kwa kina historia na utendaji wa Baba Mtakatifu Benedikto XV, na kusisitiza kwamba, kwenye kiini cha maamuzi ya Papa huyu, kuna utambuzi wa heshima kwa utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.  Baba Mtakatifu huyu, aliishi binafsi utume wa harakati za amani, sio kama kitu cha pembeni, bali kama sehemu msingi ya maisha na utume wa Kanisa. Benedikto XV alijikuta kajikita katika utafutaji amani, na hivyo kufanya suala hilo kuwa ni kipaumbele cha diplomasia ya Kanisa. Uanzilishi wake huu, unaendelezwa kwa namna ya pekee na Yohane XXIII kwa Barua ya kitume Pacem in terris, yaani Amani duniani, Evangelii nuntiandi, yaani Uenezaji Injili, ya Paulo VI, na Evangelii gaudium, yaani Furaha ya Injili, ya Papa Francisko, ambaye anaonya kwamba, changamoto ya wakimbizi ni ishara ya vita inayoelekea Ulaya, iwapo haitatafutiwa ufumbuzi.

Baba Mtakatifu Benedikto XV, anakumbana na karne ya ishirini ikiwa na kinzani nyingi na kila mtu anamtazama kwa matarajio fulani. Ni wakati ambapo inaisha tabia ya kuendekeza siasa ndani ya Kanisa, na kuboresha zaidi maisha ya kiroho na utume. Ni wazi kwamba Kanisa hata katika karne zilizotangulia, lilishuhudia umwagaji wa damu, lakini Benedikto XV, anashuhudia kwa mara ya kwanza makundi makubwa ya silaha kali yanayoteketeza watu na vitu kwa chuki kubwa, anashuhudia jinsi baadhi ya watu wa mataifa fulani fulani wanaangamizwa ili kutokomeza kabisa kizazi chao. Ndiyo sababu katika maadhimisho ya sikukuu ya kuzaliwa Bwana mwaka 1915, aliita vita hiyo kuwa ni Uteketezaji.

Maneno na vitendo vya Mababa Watakatifu huwa ni ufunguzi wa njia. Hivyo Kanisa linaamua na kuchagua, sio tu nini cha kusema, bali pia nini cha kutenda na kwa namna gani. Kanisa ni kama Huduma ya kwanza katika maisha na historia ya mwandamu. Benedikto XV anapata nguvu kubwa kutokana na uamuzi wa kutofungamana na siasa za aina yeyote, wala kutofungamana na wakuu wa taifa lolote lile. Nguvu hii na uamuzi huu, hauonekani kutambuliwa sana na wakuu wa mataifa tangu enzi hizo, lakini raia wengi wameutambua na kuuthamini. Benedikto XV hakuitazama vita kama mzigo tu na uhasi wa dini  kwa upande wa kisasa, bali aliitumia kama nafasi ya kutangaza na kutafuta amani kwa kutumia diplomasia. Mchungaji huyu wa kanisa, kwa mara ya kwanza anaanza kutazama mahusiano ya Kanisa la Roma kwa mshikamano wa karibu zaidi na Makanisa Mahalia yaliyo katika mahangaiko, mfano nchi ya Armenia, iliyoharibiwa na kunyanyaswa vibaya wakati wa vita ya kwanza ya dunia.

Kardinali Pietro Parolin anafunga hotuba yake kwa kusisitiza kwamba: Papa Benedikto XV amekuwa kwa hakika nabii wa amani. Na kutokana na unabii wake, mataifa kadhaa yalibadirika na kuanza kuheshimu utu na uhuru wa watu. Wakristo wakaanza kuongeza bidii katika mshikamano na watu waliokuwa wahitaji. Kwa sababu hiyo, ni muhimu kuifahamu historia ya Kanisa na dunia kwa ujumla, na kuchambua kwa umakini tabia na maamuzi ya Benedikto XV, ili kuonja utajiri unaotokana na wito na utume wake akiwa khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.