2016-11-13 09:12:00

Kanisa nchini Marekani: Haki Jamii & Utakatifu wa maisha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Usccb, kuanzia tarehe 14- 16 Novemba 2016 litafanya mkutano wake huko Baltimore ili kupanga sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa mwaka 2017 – 2020 kwa kujikita zaidi katika haki jamii na utakatifu wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Uinjilishaji mpya ni kati ya changamoto kubwa zinazofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kwa wakati huu, ili kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuweza kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao kwa njia ya shughuli za kimissionari.

Maaskofu wanahamasisha waamini kujenga mahusiano ya karibu na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Maaskofu wanapenda pia kukazia na kudumisha Injili ya ndoa na familia, ili kuimarisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kikristo na kiutu.

Katika mwelekeo huu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Utakatifu wa maisha ya binadamu unapaswa kulindwa na kuendelezwa tangu pale mtu anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hapa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanapaswa kulindwa na kutetewa dhidi ya wajanja wachache wanaotaka kujinufaisha kutokana na umaskini na unyonge wao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linapenda kujikita zaidi katika majiundo awali na endelevu kwa wakleri, watawa na waamini walei, ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza vyema dhamana na utume wao katika maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa. Familia ya Mungu nchini Marekani inapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini unaojikita katika ushuhuda wa imani ndani na nje ya Marekani.

Mkutano huu itakuwa ni fursa ya kupokea taarifa mbali mbali zilizokusanywa na kikosi kazi katika kudumisha amani na maridhiano nchini Marekani kutokana na matukio kadhaa ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yaliyosababisha kinzani na mivutano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama. Matukio yote haya ni nafasi ya kutafakari kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Marekani. Maaskofu wanatambua dhamana na wajibu wao wa kuhakikisha kwamba, wanatoa dira na mwelekeo utakaosaidia mchakato wa kulindana kudumisha amani na maridhiano kati ya watu kwa kujikita katika amani jamii, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa. Baraza la Maaskofu pia litatumia muda huu kuchagua viongozi wapya kwani Askofu mkuu Joseph Edward Kurt anamaliza awamu yake ya uongozi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.