2016-11-13 11:08:00

Jubilei ya miaka 100 ya Taasisi ya Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki


Ni jambo la muhimu sana kurudi Damasko, kama ilivyo muhimu kurudi Mashariki yote ya kati. Kwa ujumbe huu, ndivyo yanafunguliwa maadhimisho ya miaka 100 ya Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki, na kongamano la kimataifa lenye kauli mbiu, Damasko mche wa matumaini. Kongamano lililoanza tarehe 11 Novemba na kufungwa rasmi Jumapili, 13 Novemba, 2016.

Kongamano lililoandaliwa katika taasisi hiyo, linalenga kutoa mwanga na nuru ya matumaini kwa hali iliyopo ya Makanisa ya Mashariki ya kati leo. Kuna kilio kikubwa kutoka nchi nyingi za mashariki ya kati, zilizo katika mtafaruku na machafuko ya muda mrefu. Changamoto ya wahamiaji, imefanya makanisa mahalia ya tamaduni za miaka mingi, kugeuka na kuwa makanisa ya waliohama, yaani diaspora, na hivyo kutokuwa na uhakika wa Kanisa la siku za usoni litakuwaje.

Wananchi takribani Milioni 13.5 wa nchi ya Siria, wanahitaji msaada wa mahitaji msingi ya binadamu, milioni 5 wamekimbia kutoka Siria, na milioni 6.5 wamejazana katika mipaka ya nchi yao wakiwa wamegubikwa na hofu, wakati huo Jumuiya za kikristu zinateswa na kunyanyaswa na makundi ya itikadi kali. Kongamano la kimataifa lililofanyika katika Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki, ni nuru ya kufungua uwanja wa kukutana na kufanya mazungumzano, kwa nia ya kujenga tena Maisha na tamaduni za watu wa mashariki ya kati, kutafuta mapatano, na zaidi sana kujitafakari juu ya utambuzi binafsi na kujisikia nyumbani, mambo yatakayowezekana kwa kutazama kwa kina namna ya kuelimishana kwa siku za usoni.

Taasisi ya Kipapa ya Makanisa ya Mashariki iliundwa na Baba Mtakatifu Benedikto XV, mwezi Oktoba 1917, kwa Barua Binafsi (Motu proprio), Orientis catholici, yaani Wakatoliki wa Mashariki, miezi michache baada ya kuundwa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Mnamo mwaka 1922 Baba Mtakatifu Pius XI, aliikabidhi taasisi hiyo kwa Mapadri Wamisionari Wajesuiti ili kuisimamia.

Taasisi hii ina lengo kuu la kufanya Makanisa ya Mashariki kutambua utajiri uliosheheni katika utamaduni wao (Rej., Yohane Paulo II, Orientale lumen, yaani Mwanga wa Mashariki, Na. 4). Wakati huo huo inalenga kufanya Kanisa la Magharibi kuona pia utajiri huo ambao haufahamiki sana kwao. Baba Mtakatifu Francisko, katika kuelekea maadhimisho ya miaka 100 ya taasisi hiyo, anawaandikia wakufunzi na wanafunzi kwamba: utajiri mkubwa ulio katika utamaduni wa Makanisa ya Mashariki, unaweka uhai wa Utakatifu kwenye Liturjia, unafungua milango mipya ya utafiti wa taalimungu, na unapendekeza mtazamo wa huruma wa taratibu za Kanisa.

Hakika taasisi hiyo, ni mahali pa kuwaandaa vema kimalezi na taaluma watu wa maisha ya wakfu kutoka Makanisa ya Mashariki. Taasisi inafanya tafiti, inafundisha, na inachapisha vitabu na makala zihusuzo uhalisia na utajiri wa Makanisa ya Mashariki kwa upande wa taalimungu, liturjia, mafundisho ya Mababa wa Kanisa, historia, Sheria za Kanisa, Uandishi, lugha, Maisha ya kiroho, mambo ya kae na mahusiano ya kiekumene na kisiasa. Kwa namna hii, Kanisa linapopumua kwa mapafu mawili, yaani Kanisa la Mashariki na Magharibi, linaendana na sala ya Kristo anayeomba kwa Baba: wote wawe wamoja (Rej., Yohane 17: 11)

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.