2016-11-13 08:42:00

Jubilei ya maskini: Yote yatapita, lakini Mungu na Jirani watadumu!


Kwa wale wanaomwamini na kumtumainia Mungu, jua la haki litawazukia, kwani hawa ni watu ambao wamemchagua Mungu na kumfanya kuwa ni kipaumbele katika maisha yao hapa duniani. Hawa ndio maskini wa haki, lakini matajiri wa maisha ya kiroho mbele ya Mwenyezi Mungu. Hawa Yesu anasema ndio wale watakaorithi ufalme wa mbinguni, urithi wa Mungu. Nabii Malaki anasema watu wenye kiburi na watendao maovu ni wale aliojiaminisha na hatimaye kumezwa na malimwengu, kiasi cha kushindwa kumweka Mungu kuwa ngome ya usalama wao anayezima kiu ya maisha ya ndani.

Hii ni sehemu ya tafakari ya Neno la Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 13 Novemba 2016 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Yesu kabla ya kukabiliana uso kwa uso na Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wake, alizungumzia kuhusu uzuri wa Hekalu na mahangaiko nyakati za mwisho, pale Mwana wa Adamu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu.

Yesu aliwataka wafuasi wake kuisubiri Siku hii kwa imani, matumaini na subira badala ya kujihangaisha na udadisi usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa maisha ya uzima wa milele, mambo ambayo hata Yesu mwenyewe hakuyafurahia. Anawataka kuwa waangalifu na kamwe wasidanganywe na wahubiri wa uwongo wanaotishia maisha ya watu, watabiri wa nyota au mahubiri yanayotishia usalama na maisha ya watu, changamoto hapa ni kusikiliza sauti  ya Mungu inayozungumza kutoka katika undani wa maisha yao bila kusongwa mno na woga, wasi wasi, kinzani na migawanyiko.

Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba watakumbana na vitisho, dhuluma, mateso na hata mauaji, lakini jambo la msingi ni kuendelea kuwa na subira, imani na matumaini kwani kwa njia hii wataweza kuziponya roho zao. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu hawezi kuwasahau waja wake, kwani wao wana thamani kubwa mbele yake, kama ilivyo kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Neno la Mungu linawakumbusha wanadamu kwamba, kila kitu kinapita, mambo makuu mawili ndiyo yenye thamani kubwa katika maisha yaani: Mungu na Jirani! Haya ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha kwa kumwambata Mungu na kuonesha upendo kwa jirani!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anakaza kusema, leo hii inasikitisha kuona kwamba, kuna watu wanaogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na wengine wengi wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Lakini, binadamu ana thamani kubwa mbele ya Mungu aliyekabidhiwa dhamana ya kutunza kazi ya uumbaji, kumbe, si jambo linalokubalika hata kidogo  kuona mwanadamu ambaye ana thamani kubwa mbele ya macho ya Mungu anabezwa na kutwezwa kutokana na matatizo na changamoto mbali mbali za maisha. Maskini hawa si tena sehemu ya habari inayopewa uzito wa juu, bali ni mkia wa kufungia taarifa za vyombo vya habari!

Maadhimisho ya Jubilei kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni fursa makini ya kumwangalia mtu kama anavyomwangalia Mungu kutoka katika undani wa maisha yake na wala si yale yanayoonekana kwa nje. Mungu anauangalia moyo uliovunjika na kupondeka. Inasikitisha kuona kwamba, akina Lazaro ambao ndio maskini wa ulimwengu mamboleo wanatazamwa kwa jicho la kengeza na watu wanajidai kana kwamba hawaoni jinsi wanavyotengwa na kubezwa na jamii, jambo ambalo ni sawa na kumgeuzia Mungu kisogo!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu wanathamini vitu vinavyozalishwa badala ya kuwapenda watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Matokeo yake ni maendeleo na fursa nyingi katika maisha ya watu, lakini kwa upande mwingine kuna watu wasiokuwa na fursa hizi na wanaendelea kudidimia katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, kielelezo cha ukosefu wa haki. Haiwezekani kuwa na amani na utulivu duniani wakati kuna watu wanakufa kwa njaa, utupu na ukosefu wa amani na utulivu.

Makanisa na Madhabahu ya huruma ya Mungu, sehemu mbali mbali za dunia yamefungwa rasmi Jumapili, tarehe 13 Novemba 2016, kama sehemu ya mchakato wa kuhitimisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kamwe wasifunge macho yao mbele ya Mungu anayewaangalia jinsi wanavyowatendea jirani zao. Waamini watambue kwamba, Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, yote yatapita lakini upendo utadumu milele, changamoto ya kuwa ni watu wa imani na matumaini kwa ajili ya furaha ya maisha ya uzima wa milele. Kanisa lina waangalia maskini kwa jicho la upendo, changamoto na mwaliko wa kuondokana na masuala ya upendeleo, uchu wa mali na madaraka pamoja na kumezwa na malimwengu. Mama Kanisa anapenda kuwaangalia wale wote wanaoteseka, wanaolia na kuomboleza kwani wao ni msingi wa Injili kwa haki na wajibu, kwani wao ndio utajiri na amana ya Kanisa kama anavyokaza kusema na kushuhudia Mtakatifu Laurent. Mungu na jirani viwe ni vipaumbele vya kwanza katika maisha ya waamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.