2016-11-12 09:43:00

Malawi simameni kidete kupambana na utamaduni wa kifo!


Kanisa Barani Afrika kama chombo cha haki, amani, upatanisho linapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na itikadi pamoja na sera za utuoaji mimba, kifo laini na ndoa za watu wa jinsia moja, mambo ambayo kimsingi yanakwenda kinyume cha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mafundisho ya Kanisa kuhusu uhai wa mwanadamu ni wazi kabisa kwani tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake anapaswa kulindwa na kuendelezwa hadi pale mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Familia ya Mungu Barani Afrika anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, “Dhamana ya Afrika”, “Africae munus” kwamba, inapaswa kusimama kidete kutangaza, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa halina budi kusimama katika ukweli huu hata kama litakosa umaarufu au kujenga uhasama na makundi ya watu kwani Kanisa linatambua kwamba, liko ulimwenguni lakini si la ulimwengu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linapenda kuonesha msimamo wake dhidi ya muswada wa sheria unaotaka kuhalalisha vitendo vya utoaji mimba kisheria nchini humo jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu. Muswada huu wa sheria ulianza kuwasilishwa Bungeni tangu mwaka 2015 na sasa unataka kupitishwa ili hatimaye uwe ni sheria, lakini sheria inayokumbatia utamaduni wa kifo. Sheria hii inatoa upendeleo wa pekee kwa wanawake wanaojikuta wakiwa hatarini kuweza kutoa mimba au pale watoto wanapoonekana kuwa na kasoro katika miili yao au wanawake waliobakwa na kupachikwa mimba.

Wakati wa hija yake ya kitume nchini Malawi kwa ajili ya kutabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki Karonga, Kardinali Fernando Filoni, alionya kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Watu wana thama ni kubwa mbele ya Mungu kuliko vitu kwani hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jamii haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu.

Kutokana na changamoto ya utamaduni wa kifo kutaka kuingia kwa kasi nchini Malawi, Askofu Thomas Luke Msusa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kujikita katika Injili ya uhai na utu wema. Mapambano haya yanaungwa mkono pia na Baraza la Makanisa nchini Malawi. Wanaharakati wanaounga mkono sheria hii inayokumbatia utamaduni wa kifo wanasema inalenga kuokoa maisha ya wanawake wanaolazimika kutoa mimba huku wakiwa ufichoni kutokana na sababu mbali mbali katika maisha. Sheria ya sas anchini Malawi inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa wale wote watakaotiwa mbarani kwa kosa la kutoa mimba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.