2016-11-12 15:29:00

Huduma ya afya: Mwingiliano wa kijamii, kanuni auni & utu wa wagonjwa


Mkutano wa XXXI wa Kimataifa kuhusu magonjwa adimu na yanayoweza kupatiwa tiba muafaka ni tukio ambalo limewakusanya mabingwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kupembua changamoto hii katika mwelekeo wa: kisiasa na kijamii; kisheria na kimaadili ili kuwa na mwelekeo mpya zaidi wa kiafya na kitabibu unaozingatia na kuthamini maisha, utu na haki msingi za mgonjwa zinazofumbatwa katika dhamana ya ukarimu na mshikamano; kwa kuibua mbinu mkakati wa tiba ya upendo kwa wagonjwa husika.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinazonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 400 wanaosumbuliwa na magonjwa adimu au magonjwa yanayoweza kupatiwa tiba muafaka ambao wanakadiriwa kuwa ni zaidi ya billioni moja. Hawa ni wale wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani; mahali ambako hakuna huduma bora za afya, umaskini pamoja na ukosefu wa mahitaji msingi ya binadamu, hasa Barani Afrika na Amerika ya Kusini; bila kuyasahau maeneo ambayo yako kwenye Ukanda wa Joto Duniani.

Ukosefu wa maji safi na salama; usafi wa chakula na lishe pamoja huduma duni za kijamii na makazi hafifu ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia ongezeko la watu wenye magonjwa adimu na yale yanayoweza kupatia tiba muafaka. Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliomtumia Monsinyo Jean-Marie Musivi Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya, kwa niaba ya wajumbe Mkutano wa XXXI wa Kimataifa kuhusu magonjwa adimu na yanayoweza kupatiwa tiba muafaka. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Hayati Askofu mkuu Zygmunt Zimowsk, aliyekuwa Rais wa Baraza hili ambaye amefariki dunia mwezi Julai 2016.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto kubwa kwanza kabisa kama magonjwa ya kuambuza; tafiti za kisayansi, huduma za kitabibu, usafi wa mazingira ya huduma ya afya bila kusahau mwelekeo wake wa kiuchumi. Ni dhamana inayowawajibisha watu wengi katika ngazi ya kimataifa; viongozi wa kisiasa, mashirika ya afya kitaifa na kimataifa; wafanyakazi katika sekta ya afya; viwanda vinavyozalisha dawa za binadamu, mashirika, vyama vya kiraia, wagonjwa pamoja na watu wa kujitolea yaani waamini walei na watawa katika ujumla wao.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto inayoweza kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali pamoja na kushirikiana na Kanisa ambalo  limekuwa mstari wa mbele kuchagia mustakabali wa huduma ya afya kwa binadamu kwa kutambua kwamba linasukumwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Kristo anayejidhihirisha kuwa kama “Mgonjwa” na “Daktari” yaani Msamaria mwema. Ili wajumbe hawa waweze kutekeleza vyema dhamana yao, Baba Mtakatifu anawataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu na heshima ya binadamu, dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu; watu wenye lengo la kutaka kupata suluhu ya kimataifa, kwa kuongozwa na hekima ya moyo! Hapa kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa kisayansi na kitekolojia ili kuweza kupambana na magonjwa haya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwekeza katika sekta ya afya, ili kuwasaidia wagonjwa kama sehemu muhimu sana ya matendo ya huruma. Litaendelea kuelimisha na kuhabarisha maarifa na ujuzi mintarafu tafiti za kisayansi na huduma makini kwa wagonjwa kwa kujikita katika mantiki ya ukarimu na mshikamano katika maisha ya mgonjwa pamoja na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira, anamoishi binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya magonjwa haya na mazingira machafu ambayo yamekuwa kwa sehemu kubwa chanzo cha magonjwa ya kijenetiki, changamoto ya kusimama  kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Pili, Kanisa litaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa kuwahudumia wagonjwa wanaoishi pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya kijamii, kiuchumi, kiafya, kimazingira na kijiografia. Kanisa pia linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika haki kwa ajili ya wagonjwa ili kuwapatia huduma makini.

Baba Mtakatifu anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakazia mambo makuu matatu; mwingiliano wa kijamii kwani huduma ya afya ni jambo jema la kijamii linaloweza kuimarisha afya bora kwa watu wengi. Pili, Kanuni auni itaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuchangia kwa hali na mali katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa na tatu ni kuibua mbinu mkakati wa huduma kwa wagonjwa unaozingatia utu na heshima ya binadamu, mafao ya wengi na mshikamano. Hivi ni vigezo muhimu katika kupambana na magonjwa adimu na yale yanayoweza kupatiwa tiba muafaka, kwa kujizatiti katika upendo kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.