2016-11-11 16:16:00

Kanisa ni kwa ajili pamoja na maskini!


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unapoelekea kileleni hapo sikukuu ya Kristu Mfalme, tarehe 20 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kupokea mahujaji wa makundi mbali mbali, wanaoadhimisha Jubilei hiyo pamoja naye, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Siku ya Ijumaa hadi Jumapili, tarehe 11-13 Novemba 2016, anakutana na kusali pamoja na mahujaji maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wakiwa wanaadhimisha Jubilei yao. Katika tukio hilo, Kardinali Barbarin anatoa salaam za utangulizi kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Tangu mwanzo mwa utume wake kama Khalifa wa Mtume Petro, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha nia yake ya kufanya ling’ae Kanisa maskini kwa ajili ya maskini. Kwenye Wosia wa Kitume, alioutoa mwanzoni mwa utume wake anaandika kwamba: Kristo mwenyewe kila siku amejifanya maskini kati ya maskini, na hija yote ya wokovu wa mwanadamu inazungukwa na kuguswa na maskini. Kardinali Philippe Barbarin anamweleza Baba Mtakatifu Francisko kwamba, anachokishuhudia katika Jubilei ya maskini, ni furaha ya maskini hao kujisikia kuwa wapo katika moyo wa Kanisa, pamoja na Baba Mtakatifu. Maskini hao, hawana haja ya kukaribishwa, kwani wanajitambua kuwa ni sehemu ya udugu na Familia kubwa ya Kanisa, ambamo wao maskini ni hazina na utajiri wa Kanisa lenyewe.

Kristo anasema: maskini mko nao siku zote (Rej., Yohane 12,8). Hii inamaanisha, maskini hawana sababu ya kujionesha au kutenda kwa ajili ya wengine, bali kila muumini anapaswa kutambua, kuzoea na kuufurahia uwepo wa maskini ndani ya Kanisa, kwa sababu, maskini wanampa muumini fursa ya kuwa mfuasi wa Kristo. Hiyo ni sifa mojawapo ya mfuasi wa kweli wa Kristo, kuwa kati ya maskini akishuhudia upendo na huruma ya Mungu. Kristo anafundisha kwamba: ufanyapo karamu usialike marafiki, ndugu jamaa na matajiri ambao watakualika nawe pia, nawe utapata thawabu yako, bali alika maskini ambao hawana kitu cha kukurudishia, na hapo utapata thawabu yako mbinguni. Haya sio maneno ya kumbukumbu tu, bali ndio utume, nyumba, sala na maisha ya kila siku ya mkristo, anasema Kardinali Barbarin.

Kuna maskini wanaoishi katika nyumba kwa pamoja kama ndugu, na watu wanajitolea kuwahudumia mahali hapo. Wanasali pamoja, wanashiriki Ekaristi Takatifu pamoja, wanakula pamoja, wanashirikishana maisha yao ya zamani na ya sasa. Kwa namna hii, maskini wanajisikia kukutana na kaka na dada zao, kukutana kama marafiki. Wanaposhirikishana utajiri walio nao kila mmoja, wanakuwa katika hija moja ya kutafuta uhuru wa ndani. Kanisa linaposafiri kwa pamoja, hakuna atakayehisi utofauti wa maskini na tajiri, bali wote wanakuwa familia moja yenye lengo moja.

Sauti ya Mungu Baba ni ya msingi kuielewa katika hili, Yeye aliyempenda sana mwanae Yesu Kristo, na ndani yake kauweka upendo wote kwa wale anaowapenda. Kumbe ndani ya Kristu kunapatikana kisima cha  huruma na upendo wa Mungu. Hivyo wanavyosali “utakalo lifanyike duniani kama mbiguni”, katika sala ya Baba Yetu, kila mmoja awe tayari kuyapokea mapenzi ya Baba. Hivyo ndivyo kila mmoja atavumbua upendo wa mwingine, bila kujali umaskini wala utajiri. Juibilei ya maskini pamoja na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, inahudhuriwa na maskini kutoka nchi 22 duniani. Sala yao kubwa, ni kuwa karibu zaidi na moyo wa Yesu, nao wanamuombea Baba Mtakatifu aendelea na moyo wake wa ukweli, uwazi, na msimamo kwa mambo ya imani na kuwajali wahitaji.

Na Padre Celstine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.