2016-11-11 15:57:00

Jubilei ya maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, imekuwa ni fursa ya kuweza kukutana, kusali na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 11 Novemba 2016. Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda zilizotolewa na wawakilishi wa kundi hili na hatimaye kuwapatia neno la faraja katika shida na mahangaiko yao ya ndani.

Baba Mtakatifu anasema, umaskini ni hali ya kawaida katika maisha, lakini kuna watu maskini ambao wamepoteza ari, mwamko na matumaini ya kuota ndoto njema katika maisha. Hakuna kati yao, aliyekuwa na ndoto kwamba, siku moja wangeweza kufika mjini Roma na kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa wale waliokuwa na hamu hii ndani mwao, leo imetimia. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii lazima waendelee kuota ili siku moja waweze kuona mabadiliko ulimwenguni, hamu inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni kiini na lengo la Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni watu maskini, wagonjwa na waliokuwa wametengwa na jamii, wakawa na ndoto ya kukutana na Yesu, aliyewapatia chachu ya mageuzi katika maisha yao kwa kuwaponya magonjwa yao, kwa kuwasamehe dhambi zao pamoja na kuwapatia mahitaji yao msingi. Maskini ni mashuhuda wa watu wanaoridhika hata kwa kidogo wanachokipata katika maisha.

Kuna watu ambao kila siku wanaimba litania ya ukosefu wa chakula, dawa na huduma makini, ingawa mambo haya wanayo lakini bado hawatosheki kutokana na tamaa ya kibinadamu. Watu wajenge utamaduni wa kuona uzuri wa maisha hata katika mambo ya kawaida kwa kutambua kwamba, hata maskini ni watu wenye utu na heshima yao mbele ya Mungu. Hakuna mateso, furaha au shida inayoweza kumwondolea mwanadamu utu na heshima yake. Maskini ni watu walionyonywa na kupuuzwa na jamii, lakini bado wana utu na heshima yao na kwamba, wao ni kiini cha Injili ya Kristo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna watu wanaotumia umaskini kwa ajili ya kuwanyanyasa wengine, hali kama hii inahitaji ukombozi, ili watu kama hawa waondolewe katika mazingira haya na kuwekwa huru kabisa! Hali ngumu ya maisha na umaskini si kigezo cha kuwabeza watu. Jambo la msingi ni kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu. Kwa wale wanaoshiba na kusaza, si rahisi sana kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, vita ni kati ya mifumo mibaya ya umaskini inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo, umaskini wa hali na kipato; hali ngumu ya maisha na kwamba, kuna haja kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Inasikitisha kuona maskini kwa maskini wakitwangana ngumi, kwani kwa kawaida maskini ni wajenzi wa amani duniani, ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Dini zinapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani, kwa kuwafunda waamini wao misingi bora ya kiimani, kiutu na kijamii, ili amani iweze kusaidia kulinda na kudumisha utu wa watu.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni kwa niaba ya Wakristo ambao hawasomi tena Biblia kutambua kwamba, maskini ni kiini cha Injili ya Kristo, amewaomba msamaha pale ambapo amewakwaza au hakuwatendea kama wanavyostahili; pale waamini walipowapatia kisogo badala ya kuwasaidia. Msamaha wao kwa waamini ni maji ya baraka yanayowasafisha, ili kuanza mchakato wa ujenzi wa Kanisa makini kwa ajili pamoja na maskini. Hii inatokana na ukweli kwamba, maskini ni vyombo na mashuhuda wa Neno wa Mungu, aliyefanyika mwili, akakaa kati ya watu wake, ili kuwasindikiza kwenda nyumbani kwa Baba mwenyehuruma na mapendo. Baba Mtakatifu amewaombea maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kuendelea kuwa ndoto ya maisha bora zaidi, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu; ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.