2016-11-11 11:00:00

Diplomasia ya Kanisa inalenga: haki, amani, umoja, udugu na mafao ya wengi


Taasisi kama vyuo vikuu zina wito kutoa elimu msingi na uzamifu katika sayansi, na pia kutoa mchango wake katika masuala makubwa yanayougusa utamaduni wa mwanadamu kwa zama za sasa. Kwa utangulizi huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ametoa hotuba yake siku ya Jumatano, tarehe 9 Novemba 2016, katika ufunguzi wa mwaka wa masomo kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Lateran, kilichopo Jijini Roma.

Vyuo vikuu vya Kipapa vinatoa mchango wake kwa maisha ya Kanisa, lakini pia kwa masuala makuu na ya msingi yanayoikabili jamii ya mwanadamu, jamii ambamo Kanisa linaishi na linatenda utume wake. Masuala hayo yanakabiliwa kwenye mada zilizopo katika Nyanja za Taalimungu, Falsafa na Sheria. Wajibu huo sio mwepesi, ikizingatiwa ulimwengu wa leo ulivyo na mawasiliano ya haraka, matukio mbali mbali na uhalisia wa utandawazi, inaonekana kutoa kabisa nafasi ya kujadili na kufanya tafiti juu ya mwanadamu, uwepo wake na mahusiano.

Katika hali kama hii, anasema Kardinali Parolin, inafaa kukumbuka maneno ya Baba Mtakatifu Francisko anayesema: haitoshi kufanya uchunguzi na kuelezea mambo yalivyo, bali ni muhimu kuweka uhai katika mazingira ya mwanadamu, kwa kufanya tafiti za kweli, hivyo ni lazima kwenda katika uhalisia na kutoa mapendekezo mbadala. Katika kufanikisha hilo, ni lazima kutumia utaalamu, mamlaka na uwezo katika kuweka nguvu kazi na sadaka kila siku kwa wanafunzi na wakufunzi. Kila mmoja ajisikie wajibu wa kutafuta majibu na suluhu ya changamoto za jamii ya leo. Ni muhimu kushinda uzembe.

Kanisa linatambua kwamba dunia ya leo inaishi katika zama za utandawazi, ambapo wote wanaishi yote, kila mmoja anashiriki na anaishi kila kitu, tena kwa muda mfupi. Maisha ya kijamii na ya kisiasa yamegubikwa na utandawazi, wakati huo uhalisia wa mwandamu katika muungano wa roho na mwili, pole pole unapoteza utambuzi wake, na kuanza kujikita kwenye mwanadamu wa utandawazi. Mwanadamu anatumiwa kama kitu na hivyo kupoteza utu wake. Uhai wa mwanadamu unapangwa toka kutungwa mimba, makuzi, faida yake katika jamii, kiasi kwamba wale dhaifu kama wagonjwa na wazee wanatupiliwa mbali. Haya ni machache tu, lakini yanafungua mwanga kuona nafasi na umuhimu wa wana diplomasia ya Kanisa wanaopaswa kuwa na mtazamo tofauti ili kubadili hali za matabaka kati ya maskini na tajiri, elimu na ujinga, imani na kutojali dini, haki na dhuluma, amani na machafuzi, usalama na vita.

Kuna tatizo kubwa ambapo Jumuiya ya Kimataifa inasita kuchukua hatua, kila mmoja anakwepa kujihusisha na baadhi ya mambo mfano ugaidi, kwa kukwepa matatizo au kupoteza masilahi fulani. Katika hali ya namna hii, nafasi ya diplomasia ya Kanisa inaonekana kuwa ya lazima na muhimu, ili kutetea haki msingi za mwandamu, haki ya kimataifa, na maisha bora ya Familia ya mwanadamu kwenye Nyumba ya wote. Mfano suala la wahamiaji leo linalosababishwa na uonevu na uvunjwaji haki na machafuko sehemu mbali mbali, muda sio mrefu wahamiaji wataongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.Diplomasia ya Vatican inawahimiza wote kuchukua hatua na kuwajibika kukabili hali halisi baada ya utandawazi. Baba Mtakatifu Francisko, anawakumbusha wana diplomasia wa Kanisa kuwa: wao ni wachungaji walio na uwezo wa ndani wa kumshuhudia Kristo katika utendaji wao. Kwa sababu hiyo, Kanisa lina mahusiano ya kidiplomasia katika mataifa 179 na taasisi 31 za kimataifa na kanda. Vivyo hivyo Vatican inapokea mabalozi kutoka mataifa mengine ili kudumisha mahusiano na mazungumzano endelevu.

Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na mataifa mengine yanafanyika kwa uvumilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna ugumu mkubwa, kwa kuwa kuna matumaini ya Familia bora ya wanadamu kwa baadae. Shughuli za kidiplomasia zinakuwa nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kushawishi katika Jumuiya na maisha ya Kimataifa. Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya Amani, haki na mafao ya wengi. Diplomasia ya Kanisa sio upendeleo kwa Kanisa, bali ni haki ya msingi ambayo Kanisa inayo, na hivyo katika Jumuiya ya Kimataifa, Kanisa lina haki sawa kama vyombo na jumuiya zingine wanachama. Kwa zama hizi, ni wajibu wa Kanisa kutafuta mahusiano ya Amani kati ya mataifa, wakati likizingatia lengo la mwisho, yaani wokovu wa roho za watu.

Monsinyo Battista Montini, mkufunzi wa diplomasia ya Kanisa kwa 1930-1938 alisema: iwapo diplomasia za mataifa zina lengo la kutafuta amani na utulivu katika Jumuiya za Kimataifa, diplomasia ya Kanisa inakwenda mbele zaidi, ili kupalilia udugu kati ya jumuiya hizo. kwa namna hii, ni jibu sahihi kwa mahitaji ya makubaliano kati ya watu na uhuru wa Kanisa, hivyo kufungamanisha chanzo cha mwanadamu, haki na uhuru wake. Mafanikio ya hivi karibuni katika diplomasia ya Kanisa yanaonesha lengo hilo pana la maisha bora na ya Amani kwa kila mmoja, na wokovu wa roho za watu. Mfano makubaliano ya Palestina na Vatican yaliyofikiwa tarehe 26 Juni 2015, yanalenga kanuni za kuishi pamoja kati ya watu wa asili na dini tofauti katika Nchi Takatifu. Mafanikio ya mahusaino ya serikali za Cuba na Marekani, ambapo Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia barua binafsi wakuu wa nchi hizo. Bila kusahau pia makubaliano kati ya serikali ya Colombia na wapiganaji wa msituni, yaliofikiwa hapo Septemba 27, 2016, ili kuleta Amani nchini humo.

Utafutaji wa amani unahitaji ujasiri wa kukubali mazungumzano na kuheshimu wengine, ujasiri wa kuwa mkweli na muwazi. Amani ya kweli itapatikana kwa kuzingatia mipaka ya kitamaduni na kuweka mbele maendeleo ya jumla ya mwanadamu. Kanisa kupitia diplomasia yake, litaendelea kutetea ufahamu wa maisha ya mwanadamu yanayofunguka kumwelekea Mungu, kuhangaika ili Amani iweze kupatikana, maendeleo yafikiwe, na tunu msingi za binadamu na haki zake zipate kulindwa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.