2016-11-10 14:55:00

Umoja wa Kanisa ni hitaji la imani na zawadi katika utofauti!


Majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo ni kati ya vipaumbele vya kwanza vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa mwaka huu, Baba Mtakatifu amepata faraja ya kuweza kushiriki kwa karibu zaidi mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani na nje ya Roma, wakati wa hija zake za kitume. Ni hamu ya moyo wake kuona Wakristo wote wakiwa wameungana chini Kristo ya mchungaji mkuu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, hata Wabatizwa wengine wataweza kumuunga mkono katika utekelezaji wa nia hii njema miongoni mwa Wakristo.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 10 Novemba 2016 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Pamoja na mambo mengine amekazia kuhusu umuhimu wa umoja wa Kanisa kama hitaji muhimu sana la kiimani. Amekumbusha kwamba, umoja wa Kanisa si matunda, juhudi na bidii za binadamu, bali ni zawadi kutoka juu. Umoja wa Kanisa haumaanishi kuwa sawa katika mambo yote na wala si kuyameza Makanisa mengine.

Baba Mtakatifu anasema, Umoja wa Kanisa ni hitaji muhimu sana la kiimani kama njia ya kumwilisha upendo na ufuasi wa Kristo kama kielelezo makini cha Fumbo la Utatu Mtakatifu na ushuhuda wa imani na mapendo kwa Kristo Yesu aliyetumwa na Baba wa milele na kwa njia ya Roho Mtakatifu, Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kati ya watu. Waamini wajitahidi kuifahamu Injili ili hatimaye, waweze kuwa wamoja na kuishi na Kristo.

Huu ni mchakato wa wongofu wa mtu binafsi na Jumuiya ya waamini katika ujumla wake, ili kuweza kufanana na kuishi kama Kristo Yesu, ili kuendeleza mchakato wa umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo. Haya ni mambo msingi yanayoendelea kupewa msukumo wa pekee na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika shughuli na mikakati yake. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuwa macho na makini, ili kamwe wasichanganye mitindo ya umoja ambayo badala ya kuleta umoja itakuwa inakinzana na asili pamoja na kiini chake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Umoja wa Wakristo si matunda na nguvu ya mahusiano ya kidiplomasia yanayofanywa na Mama Kanisa, bali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto ni kuipokea na kuimwilisha zawadi hii katika umoja wa Kanisa unaoonekana. Hii ni hija inayofumbata: taratibu, mwendo na mapumziko. Safari hii inahitaji subira, uvumilivu na ushupavu; bidii na dhamana; mambo ambayo hayawezi kufutilia mbali kinzani na tofauti zilizopo kwani katika mwelekeo kama huu kunaweza kuibuka hali ya kutoelewana.

Umoja unaweza kumwambata mtu anayedhamiria kufanya hija ya maisha ambayo kwa wakati huu, lengo hili linaweza kuonekana kana kwamba, liko mbali sana. Lakini mwamini anayejibidisha katika hija hii ya maisha anafarijika na uzoefu na nia njema ya kutaka kujenga umoja katika misingi ya furaha hata kama umoja huu haujafikiwa, kwani pale wote wanapofanikiwa kuweka kando maamuzi mbele wanatambua kuwa wote wanatindikiwa upendo wa Mungu; ni wa dhambi na kwamba wanahitaji kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu iliyofunuliwa na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, umoja wa upendo ni hali halisi miongoni mwa waamini ambao wanatangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, kwa kushuhudia upendo kwa wote. Kimsingi, umoja wa Wakristo unajengekeka kwa kutembea kwa pamoja kwani wanapaata nafasi ya: kukutana, kusali, kushirikiana katika kutangaza na kushuhudia Injili pamoja na kutoa huduma ya upendo kwa maskini. Tofauti za Kitaalimungu na Kikanisa zinazoendelea kuwagawa Wakristo zitaweza kuvukwa kwa kutembea pamoja huku wakiwa wamejisalimisha kwa Roho Mtakatifu atakayewawezesha kuungana kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Umoja wa Wakristo unatambua: Mapokeo ya kitaalimungu, kiliturujia, maisha ya kiroho na sheria za Kanisa kuwa ni utajiri mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa na wala si mambo yanayohatarisha umoja na mafungamano ya Kanisa. Kutaka kufisha tofauti hizi msingi ni kwenda kinyume cha matakwa ya Roho Mtakatifu anayetaka mambo yote haya kama sehemu ya utajiri wa umoja wa Kanisa. Ni dhamana ya majadiliano ya kiekumene kuheshimu tofauti halali kati ya Makanisa kwa kujitahidi kuvuka vikwazo vinavyokwamisha umoja wa Kanisa mintarafu utashi wa Mungu. Hii ni dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote.

Baba Mtakatifu mwishoni anasema kwamba, Umoja wa Wakristo haupanii hata kidogo kurudi nyumba kiasi hata cha kupoteza historia ya imani au kuvumilia wongofu shuruti. Jambo la msingi ni kuangalia kwa kina na mapana mambo yale yanayowaunganisha Wakristo yaani: Biblia Takatifu na waungama imani wa Mitaguso mikuu ya Kanisa, ili kutambuana na kuwa ni watu wanaomwamini Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi,  watu wanaojitahidi kutii Maandiko Matakatifu yanayowataka kuwa wamoja katika Kristo Yesu. Uekumene wa kweli unatoa kipaumbele cha kwanza kwa Neno la Mungu linalopaswa kusikilizwa, kupokelewa na kumwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa walimwengu. Kumbe, Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuungana ili kutangaza na kushuhudia kwa pamoja Habari Njema ya Wokovu.  Tamko la Makanisa ya Kiekumene lililotolewa kunako mwaka 1952 linakazia umoja na mshikamano isipokuwa kwa mambo ambao yanaendelea kusababisha kinzani, ili yaweze kushughulikiwa tofauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.