2016-11-10 07:00:00

Mkutano wa Jukwaa la Wakatoliki Kitaifa Zambia


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuanzia tarehe 7 – 10 Novemba amekuwemo nchini Zambia kushiriki katika matukio mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa. Jumatano tarehe 9 Novemba 2016 ameshiriki katika ufunguzi wa Jukwaa la Wakatoliki  Kitaifa Zambia lililojumuisha wajumbe mbali mbali kutoka katika familia ya Mungu nchini Zambia.

Kardinali Filoni amewapatia wajumbe wote hawa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwashukuru na kuwapongeza kwa jinsi wanavyojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima! Familia ya Mungu nchini Zambia inaadhimisha Jubilei ya miaka 125 ya uwepo na huduma ya Kanisa Katoliki nchini Zambia, kielelezo cha ukomavu wa Kanisa na matunda yake yanaonekana katika maisha na utume wa Kanisa.

Jambo kubwa la kujivunia ni ongezeko kubwa la miito ya Kipadre na kitawa kutoka Zambia, matunda ya Wamissionari wa Afrika na Wayesuit waliojitosa kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wamissionari hawa walikumbana na magonjwa na hatari mbali mbali za maisha, lakini wakasimama kidete, leo hii matunda ya kazi na jasho lao yanaonekana wazi, Zambia imebadilika na tunu msingi za Kiinjili zinaendelea kushuhudiwa na wengi, changamoto ya kuendelea kuwa macho na waaminifu kwa mafundisho tanzu ya Kanisa.

Familia ya Mungu nchini Zambia ikumbuke kwamba, inashirikishwa na Kristo Yesu katika dhamana ya kuendeleza kazi ya Uinjilishaji inayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo thabiti cha imani. Kwa njia ya mshikamano na umoja wa kitaifa, Zambia inaweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya watu wake. Kwa mfano: ukame, ukosefu wa fursa za ajira, umaskini, magonjwa pamoja na ukabila. Katika mapambano kama haya, wananchi wa Zambia hawana sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa, bali kuendelea kujiaminisha mbele ya Mungu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kardinali Filoni, anaitaka familia ya Mungu nchini Zambia, kujikita katika maisha ya sala, ili kuweza kukutana na Kristo Yesu, tayari kushiriki katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa. Watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana katika mchakato mzima wa Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa kwa njia ya sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji. Lengo ni kutamadunisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kujenga familia imara na thabiti zinazofumbwa katika Sakramenti ya Ndoa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.