2016-11-10 15:17:00

Kitabu cha mahubiri na hotuba za Papa Francisko 2005 - 2010


Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kawaida hana kumbu kumbu ya mahubiri yaliyopita, kwani daima anajitahidi kusoma alama za nyakati ilikuweza kuwalisha waamini ujumbe wa Neno la Mungu kadiri ya mazingira. Mahubiri yanapaswa kuwasaidia waamini katika safari ya maisha yao ya kiroho na kimwili, ili kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Majandokasisi wanapaswa kufundwa vyema wanapokuwa kwenye malezi, ili kuwasaidia waamini wao kulitafakari, kulifahamu na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao watakapofikia Daraja Takatifu la Upadre.

Hata pale panapokuwepo na umati mkubwa wa waamini, lengo ni kuweza kumfikia mwamini mmoja mmoja. Mahubiri yamlenge na kugusa moyo wa mwamini katika uhalisia wake na hapa mhubiri anaweza kusema, kweli nimelifikisha Neno la Mungu kwa watu wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapendi sana kusoma mahubiri, kwani yanamnyima nafasi ya kuwaangalia waamini machoni mwao! Lakini, kutokana na hali halisi, inambidi kusoma mahubiri yake, lakini kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kila siku anajimwaga bila kutumia karatasi, anawashikirisha watu kile kinachobubujika kutoka katika undani wa tafakari na maisha yake!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya katika mahojiano maalum na Padre Antonio Spadaro kuhusu mahubiri na hotuba zake alizozifanya wakati akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, nchini Argentina, kati ya mwaka 2010, 2007, 2006, 2005 ambazo kwa sasa zimekusanywa pamoja na kuwa ni kitabu kinachojulikana “Machoni pako kuna neno langu” Kitabu ambacho kimetafsiriwa na Marisa Patarino.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda kuzungumza na watu moja kwa moja bila kufanyiwa tasfsiri, lakini anatambua pia kwamba, hana uwezo wa kuzungumza lugha nyingi duniani, kumbe anahitaji msaada wa wakarimani. Mahubiri yake anasema ni matunda ya mafungo ya maisha ya kiroho yanayomsaidia katika majiundo yake ya maisha ya kiroho hasa mafungo ya kiroho ya Mtakatifu Inyasi ni shule endelevu katika mahubiri na mara nyingi anachota hekima na busara kutoka humo! Mhubiri anapaswa kuwa na moyo wa kichungaji, ili kuwafikia watu wake!

Baba Mtakatifu anasema, kuna tofauti kati ya mahubiri na hotuba! Mahubiri ni muhtasari wa tafakari ya Neno la Mungu linalofumbatwa katika sala, ushuhuda wa maisha na busara za Mababa wa Kanisa. Anasema, katika maisha yake, amejenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye kufanya rejea ya Masomo kwa siku inayofuata. Kwa maneno mengine, anahitaji muda wa kujiandaa ili kuweza kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa watu anaowakusudia. Katika mazingira ya shida na magumu ya maisha, huko Buenos Aires aliweza kufikisha ujumbe wa imani, matumaini na mapendo. Alikuwa anasikiliza shuhuda za maisha ya watu na kuzimwilisha katika mahubiri na hotuba zake, kiasi cha kuacha mguso na mvuto wa pekee kwani Neno la Mungu linakita mizizi yake katika akili, nyoyo na maisha ya watu! Alitumia muda mrefu kwenye kiti cha huruma ya Mungu na hapo watu wengi wakatubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao. Lakini haya ni matunda ya mahubiri safi yaliyoandaliwa kwa kina na mapana; mahubiri yanayogusa watu katika undani wao. Mahubiri na mashauri ya maungamo, yalikuwa ni faraja kwa watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha, kiasi cha kujenga imani na matumaini ya maisha bora baada ya kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti zake.

Kama Paroko alipenda kufundisha Katekesi ambayo kimsingi ni muhtasari wa imani ya Kanisa, Sakramenti, Maisha adili yanayofumbatwa katika Amri za Mungu na maisha ya Sala kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu! Alifurahia kuwafundisha watoto Katekesi kwa lugha rahisi na hiyo ikawa ni dira na mwongozo wao wa maisha! Anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliyetangaza na kuzindua Mwaka wa Imani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ilikuwa ni fursa ya kupitia tena na tena nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema hata wanasiasa nao wanapaswa kufundwa katika Neno na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kweli siasa iweze kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, daima kwa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Alijitahidi kuwa na majadiliano na waamini wa Makanisa ya Kipentekoste kwani hawa walikuwa wanalitafuna Neno la Mungu vyema zaidi ikilinganishwa na Wakatoliki wengi! Baba Mtakatifu anasema anapenda kujisomea ili aweze kuhubiri kwa kutumia milango yote ya fahamu ili kuweza kufikisha ujumbe wake, daima akijitahidi kuwa karibu na watu wake. 

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuandaa vyema mahubiri yao kama alivyokazia pia kwenye Wosia wake wa Kitume, Furaha ya Injili, ili kweli Neno la Mungu liendelee kuwa hai na kuwafunda waamini katika maisha yao. Mahubiri yawasaidie waamini kufanya mang’amuzi ya maisha mintarafu mwanga wa Injili kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa. Matukio yote haya yanabeba ujumbe mzito katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya historia ya ukombozi wa mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.