2016-11-09 14:52:00

Vatican yampongeza Rais mteule Donald Trump wa Marekani


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasaidia kung’arisha upendo na huruma ya Mungu ulimwenguni kwa njia ya madiliano, ukarimu ushirikiano na mshikamano wa kidugu. Kardinali Petro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akizungumzia kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Marekani ambako Bwana Donald Trump ameibuka kidedea anasema, kuna haja ya kuheshimu utashi ulioneshwa na wananchi wa Marekani kwa njia ya kidemokrasia, ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Marekani, kumekuwepo na ushiriki mkubwa wa wapiga kura!

Kardinali Parolin, anapenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kutuma salam zake za pongezi na matashi mema kwa Rais mteule Donald Trump. Anamwombea ili Mwenyezi Mungu aweze kumwangaza na kumtegemeza katika utumishi wake kwa wananchi wa Marekani; kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza duniani anasema Kardinali Parolin, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana na wote ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa duniani pamoja na kudhibiti kinzani na mipasuko inayojitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.