2016-11-09 15:09:00

Matendo ya huruma: Kutembelea wagonjwa na wafungwa!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa waamini kuweza kutafakari kwa kina matendo ya huruma: kiroho na kimwili, tayari kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama kielelezo cha imani tendani: Jumatano, tarehe 9 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa katekesi yake amepembua kuhusu umuhimu wa kuwatembelea wagonjwa na wafungwa magerezani. Maisha na utume wa Yesu katika kipindi cha miaka mitatu ya mwisho wa uhai wake hapa duniani, alijielekeza zaidi katika kukutana na watu na akaonesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa walioponywa magonjwa yao. Yesu alijionesha kuwa ni jirani mwema kwa uwepo na nguvu yake ya kuponya na kuokoa, ndiyo maana Mama Kanisa pia anawahimiza watoto wake kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo kwa kuwatembelea, kuwasaidia na kuwafariji wagonjwa na wafungwa magerezani.

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu ambao uhuru wao umedhibitiwa kutokana na hali wanayokabiliana nayo katika maisha na kwa njia hii, wanatambua na kuonja thamani ya watu wanaowatembelea ili kuwafariji, kuwatazama na kuwahudumia katika upendo. Waamini watambue kwamba, Yesu amewakirimia uwepo wa kuwa huru kwa kiasi fulani dhidi ya magonjwa au kufungwa gerezani. Huu ni uhuru unaobubujika kutokana na mchakato wa waamini kukutana naye na hivyo kubeba uzito wote wa hali ya binadamu.

Katika matendo haya ya huruma: kimwili, Mwenyezi Mungu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika kushirikishana na wale wanaojisikia kuwa wapweke katika maisha yao, hususan wagonjwa na wafungwa. Katika ulimwengu mamboleo, watu wengi wanajisikia kuwa wapweke sana wanapokumbana na magonjwa. Kumbe, kuwatembelea wagonjwa kunawapatia nafasi ya faraja, jambo ambalo wakati mwingine ni dawa ya upweke. Tabasamu na mambo ya kawaida kabisa katika maisha ya mwanadamu, yanaweza kumsaidia mgonjwa kujisikia kuwa yuko kati ya watu na anapendwa na kuthaminiwa licha ya hali yake kitandani.

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwatembelea, kuwahudumia na kuwafariji wagonjwa majumbani mwao na hospitalini. Hii ni huduma ambayo haina malipo hata kidogo. Huduma hii inapotekelezwa kwa nia njema inakuwa ni kielelezo makini chenye mvuto na mguso wa huruma ya Mungu. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanawasindikiza wagonjwa katika shida na mahangiko yao na kamwe wasiwaache pweke, kwani hata wao wanatajirishwa kwa kuonesha uwepo wao wa karibu kwa wale wanaoteseka. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hospitali ni makao makuu ya mahangaiko ya mwanadamu, lakini pia ni mahali ambapo nguvu ya huruma na upendo vinawasaidia wagonjwa kupata faraja katika mahangaiko yao. Kwa wafungwa, Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata hawa Yesu aliwakumbuka katika maisha na utume wake!

Papa anawataka watu kuondokana na tabia ya kujinyakulia mamlaka ya kuwahukumu wengine kwani hawana vigezo sahihi. Ni kweli kabisa kwamba, mfungwa gerezani amevunja sheria na hivyo kushindwa kuishi kwa ustaharabu. Gerezani, mfungwa anatumikia adhabu yake, lakini ikumbukwe kwamba, hata katika mazingira yote haya, bado anapendwa na Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu anayeweza kuingia katika dhamiri yake na kuona ni kwa jinsi gani mfungwa huyu anavyoteseka pamoja na kusikitika kutokana na makosa aliyotenda!

Wakristo wawasaidie watu kutambua dhambi na makosa yao, tayari kuchunguza dhamiri na kuanza safari ya toba na wongofu wa ndani. Ukosefu wa uhuru kamili ni kati ya adhabu kubwa ambazo mwanadamu anaweza kupata hapa duniani. Hali hii inaweza kufikia hatua mbaya kabisa, ikiwa kama mazingira ya magereza ni hatarishi kwa usalama, utu na heshima yao kama binadamu. Changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika mazingira kama haya ni kusimama kidete kutafuta mbinu za kuweza kuwarejeshea tena wafungwa hadhi na utu wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuwatembelea wafungwa magerezani ni tendo la huruma kimwili, linalopata umuhimu wa pekee kwa wakati huu kutokana na tabia ya watu kujinyakulia wajibu wa kuwa mahakimu wa jirani zao. Kusiwepo na mtu anayemnyooshea jirani yake kidole, bali wote wajitahidi kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kushirikishana na kuheshimiana. Kuna mambo mengi ambayo yanawapelekea watu kutenda kinyume cha sheria na matokeo yake, wanajikuta wakiwa gerezani.

Katika mazingira na changamoto mbali mbali za maisha, Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuonesha upendo na uwepo wake wa karibu kwa wafungwa, ili huruma ya Mungu iweze kutenda muujiza. Ameshuhudia wafungwa wakimimina machozi utadhani bomba la maji limekatika, kwa vile tu, wamepokelewa jinsi walivyo na kuonjeshwa huruma na upendo! Mwishoni Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, hata Yesu na Mitume wake, walikiona cha mtema kuni gerezani. Simulizi la Mateso ya Yesu linaonesha jinsi gani alivyokamatwa kwa nguvu, akaburuzwa mahakamani kana kwamba, ni mhalifu wa kutupwa; akadhihakiwa na kubezwa, akacharazwa mijeledi, akavikwa taji la miiba na hatimaye, akatundikwa Msalabani.

Lakini, Yesu alikuwa ni Mwenyehaki wala hakuna hila ndani mwake. Mtakatifu Petro na Paulo walionja pia adha ya kukaa gerezani. Lakini hata katika mazingira kama haya ya gereza, Paulo mfungwa wa Kristo aliendelea kutangaza na kushuhudia Injili. Katika hali ya upweke, Paulo, alitamani kuona baadhi ya waamini na marafiki zake, wakimtembelea gerezani. Baba Mtakatifu anahitimisha katekesi yake kwa kusema kwamba, matendo ya huruma kiroho na kimwili ni hazina ya miaka mingi na bado yana mguso na mashiko hata kwa nyakati hizi, changamoto ni kuondokana na hali ya kutowajali wengine na badala yake, watu wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, ili kuwarejeshea watu wengine furaha na utu wao uliopotea kutokana na sababu mbali mbali!

Baba Mtakatifu amewapongeza Mapadre wa Madonda Matakatifu ya Yesu wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao. Anawakumbusha waamini kwamba, wanapopitia katika Lango la huruma ya Mungu, hapo wana uhakika wa kuingia katika huruma ya Mungu inayowakumbatia, inayowaganga, kuwaponya na kuwasamehe dhambi zao. Tarehe 9 Novemba, Kanisa limeadhimisha Kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kwa ajili ya kuwaomba waamini kumsindikiza Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka zao, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Wagonjwa waonje uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.