2016-11-09 07:52:00

Majiundo makini yanajikita katika: Neno, Sala, Sakramenti na Ibada!


Huduma ya kutafuta, kukuza, kupalilia na kulea miito ni wajibu wa Kiinjili ambao walezi wote wanaupokea kutoka kwa Kristo, na ni huduma inayokua na kupyaishwa kwa kukutana na Kristo kila siku katika Neno lake, Sala, na Sakramenti. Mahusiano kati ya Kristo na walezi yanapaswa kupaliliwa, na kukuzwa siku hadi siku. Kwa namna hii, walezi hubadilika na kukua kiroho, na huweza kuwaonjesha wengine furaha ya matunda hayo (Rej., Evangelium Gaudium, Furaha ya Injili, n. 8). 

Kwa utangulizi huo, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekliti wa Baraza la Kipapa la Uinjilihaji wa watu, na mjumbe maalumu wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Malawi, amewahutubia walezi wa waseminari kuu ya Mt. Dominiko, ya Lusaka, Zambia, siku ya Jumanne, tarehe 8 Novemba, 2016. Ni muhimu sana kwa walezi na mapadri wote kujikita katika sala, kwani maisha ya ukuhani yanapata lishe bora kutoka kwa Roho wa Mungu, ambaye huwaongoza katika njia thabiti ya utakatifu na ukarimu. Anayepoteza moyo wa sala, anaanza kupoteza kumbukumbu ya nini Mungu kamtendea katika maisha yake.


Kardinali Fernando Filoni kawakumbusha pia kwamba: maisha ya upadri yanafumbatwa katika useja, ambayo ni zawadi kutoka kwa Kristo mwenyewe, aliye kichwa cha Kanisa. Hivyo useja unapaswa kukumbatiwa kwa furaha na uhuru, huku kila mmoja akijiunda kila siku, kwa kuzingatia pia changamoto zinazoendana na maisha ya useja. Mapadri na waseminari wakuze moyo wa urafiki na udugu hasa kwa maisha ya jumuiya, ili kupata kufarijiana na kutiana nguvu wakati wa changamoto na kuepuka vishawishi.

Amewaalika kukuza zaidi nafasi nyingi za kukutana na waseminari katika kuabudu Ekaristi takatifu, kusoma na kutafakari Neno la Mungu na sala kwa ujumla. Wazingatie kwa umakini Nyanja za kisaikolojia na kiutu, ili waseminari waandaliwe kwa namna bora zaidi. Wakumbuke kwamba, wanaandaliwa kuwa watumishi wa Neno la Mungu na sio wahubiri wa siasa. Hivyo maelekezo yao na mafundisho yao yalenge katika kumkomboa mwanadamu katika maisha ya kila siku, hata wanapoongelea masuala ya siasa. Kardinali Fernando Filoni amewashukuru walezi hao wa seminari kwa huduma yao njema na ya kujitoa, na kawatia moyo kuendelea na utendaji wa namna hiyo, kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, Mt. Yohane Maria Vianney na Watakatifu wote wa Afrika.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.