2016-11-09 09:22:00

Jubilei ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na shukrani!


Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Upadre hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka kwa Wakleri kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko!

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 ya Upadre, wakati Padre Adamu Mmbando na Padre Atilio Mnyenyelwa walipokuwa wanamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Daraja Takatifu la Upadre. Ibada hii ilifanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma.

Askofu mkuu Kinyaiya ameikumbusha familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma, kwamba, maadhimisho ya Jubilei ni tendo la toba, wongofu wa ndani, msamaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Umefika wakati kwa waamini kuachana na maadhimisho ya Jubilei kwa mazoea, bali wanapaswa kuzingatia maana yake ya ndani, ili kweli waweze kufaidika na neema pamoja na baraka inayotolewa na Mwenyezi Mungu katika maadhimisho haya.

Jubilei ni tendo la shukrani kwa neema na baraka ambayo Mungu anawakirimia waja wake katika vipindi vya miaka 25, 50, 75, 100 na kuendelea. Lakini pia ni kipindi cha kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika vipindi hivi, tayari kutubu, kuongoka na kuambata huruma ya Mungu. Waamini wanapaswa kuzingatia Mapokeo na imani ya Kanisa na kamwe wasiwe ni vichokoo vya mabadiliko na maendeleo kasi ya sayansi na teknolojia, vinginevyo wanaweza kujikuta kwamba, wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kiroho.

Askofu mkuu Kinyaiya amewataka Mapadre wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 25 kufanya toba na kumwongokea Mungu, huku wakiomba huruma na upendo wake, ili aweze kuwakirimia tena nguvu ya kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya, tayari kuwatangazia watu wa Mungu Injili ya furaha, imani na matumaini. Ni kipindi cha shukrani kwa karama na mapaji ambayo kweli Mungu amewakirimia watu wake: kwa zawadi ya uhai na wito wa Kipadre, tayari kutoa huduma makini kwa Watu wa Mungu.

Askofu mkuu Kinyaiya amewataka Mapadre kutoridhika kwa mafanikio waliyopata katika maisha, bali waendelee kuboresha maisha na huruma yao kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Dodoma. Amempongeza Padre Atilio Mnyenyelwa, kwa huduma ya kuhubiri ambayo imemsaidia kuwatangazia watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya mafungo ya maisha ya kiroho na makongamano ya kikanda na kitaifa.

Askofu mkuu Kinyaiya amempongeza Padre Adam Mmbambo kwa huduma makini ya uongozi kama Gombera na Paroko na kwamba, wanapaswa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa na watu wanaowazunguka. Waamini Jimbo kuu la Dodoma wametakiwa kuendelea kumlilia Mungu kwa sala, sadaka na majitoleo yao, ili Mungu aweze kuwapatia watenda kazi waaminifu, wachapakazi na watakatifu, watakaokuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa maisha na majitoleo yao.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dodoma, itoe kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwajibika barabara katika maisha na wito wake. Waamini wawe wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza kutekeleza mapenzi ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku sanjari na kupambana na changamoto za maisha zinazoendelea kujitokeza Jimbo kuu la Dodoma, hasa wakati huu Serikali ya awamu ya tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli inapoendelea kujizatiti kuhamia Dodoma kama sehemuya utekelezaji wa ndoto ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba taifa, kwa takribani miaka 50 iliyopita!

Na Rodrick Minja, Jimbo kuu la Dodoma na

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.