2016-11-07 09:49:00

Tumechelewa sana, sasa tuwajibike kutunza mazingira!


Umewadia wakati wa kuzitazama nyuso za wanadamu wanoathirika na kuhangaika kutokana na makosa ya wengine ya kutojali mabadiliko ya tabia nchi. Sio suala la kutafuta ni kosa la nani, wala sio suala la kujiuliza iwapo inafaa kubadilika na kwa sababu gani, na wala sio suala la kujihoji nani aendelee kunufaika au inawezekanaje kupunguza madhara hayo. Ni suala la kutambua kwamba linaumiza na kuangamiza binadamu wote, na hasa wanyonge na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Patriaki Bartolomeo I, Kanisa la Kiorthodox la Constantinopoli, anaowaandikia Baraza la Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi, linalokutana tena Marrakech, Morocco kuanzia tarehe 7 – 18 Novemba 2016.

Ni jambo la kufurahia kuona kwamba, Baraza hilo linakutana ili kujadili na kutafuta suluhu kufuatia mabadiliko ya tabia nchi. Ni mambo mengi yaliyofanyika mpaka sasa tangu harakati za pekee zilipoanza mwaka 1992 kwa mkutano wa Rio di Janiero, Brazil. Hata hivyo maendeleo yaliyopatikana mpaka sasa bado ni kiduchu. Ni muhimu sasa kuhimiza mataifa yote kuzingatia maamuzi yanayotolewa na mikutano mbali mbali kimataifa ili kupeuka uharibifu na machafuko unaotokea. Mabadiliko hayo ya tabia nchi, yanauhusiano mkubwa pia na machafuko, umaskini na uhamiaji, anasema Patriaki Bartolomeo I.

Hewa chafu na hatari anayovuta binadamu leo, inapaswa kupunguzwa na zaidi kubadilishwa ndani ya miongo miwili. Hivyo anaonya vikali mataifa na watu binafsi wanaoendelea kuendekeza uchumi unaopatikana kwa uchafuzi wa hewa anayovuta mwanadamu. Ni jambo lisilofikirika kwa akili sahihi, kuona serikali inayojitetea kwa kuwaumiza na kuwatesa raia wake, au vivanda vinavyowafanya watumiaji wa bidhaa kuwa wahanga wa matokeo ya uendeshaji wa viwanda hivyo.

Patriaki Bartolomeo I anawaalika wote kujiuliza wanakuwa na moyo mgumu kiasi gani wa kuendelea kutolea sadaka uhai wa watu sababu ya faida za kiuchumi, na ni kwa gharama gani wanataka kuharibu na hata kutokomeza uumbaji wa Mungu. Ni mwaliko wa unyenyekevu na upole, kutilia maanani na kufanyia kazi maamuzi waliyokubaliana Baraza la mataifa la mabadilko ya tabia nchi walipokutana Paris, Ufaransa.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili 6 Novemba 2016 amekumbusha kwamba, Itifaki ya Mkataba wa Paris, kuhusu mabadiliko ya tabianchi umeanza kutekelezwa na Jumuiya Kimataifa, changamoto na mwaliko kwa watu wote kushirikiana na kushikamana katika kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote. Uchumi unapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ili kujenga na kudumisha haki na amani. Baba Mtakatifu amegusia pia mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaoanza, Jumatatu tarehe 7 Novemba 2016 huko Marrakech, Morocco unaopania pamoja na mambo mengine, kutekeleza Itifaki ya Paris. Mchakato huu unapaswa kuongozwa na dhamiri ya uwajibikaji kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.