2016-11-07 08:34:00

Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Maisha: Kudumisha uhai na utu wa mtu!


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 8 Oktoba 2016 amepitisha kanuni mpya za uendeshaji wa taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Maisha. Kanuni zitakazotumika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia sasa. Taasisi hii ilianzishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, kwa Motu Proprio, yaani Barua binafsi ya Baba Mtakatifu, Vitae mysterium, Fumbo la maisha. Lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii itakuwa na dhamana ya kutafiti,  kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbali mbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani!

Taasisi hii itakuwa ni dhamana na wajibu wa kufanya tafiti za kitaaluma na kisayansi, ili kusaidia kusimama kidete kulinda na kutetea na kudumisha maisha ya binadamu. Itakuwa na kazi ya kusaidia kuwafunda waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika utamaduni wa maisha mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni wajibu wa taasisi katika hali ya uwazi na kwa haraka, itapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Taasisi ya Kipapa ya Maisha, itawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumbaoni mwa mama yake  hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Ni wajibu wa taasisi hii kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu; kwa kuendeleza tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili, ili kudumisha Ekolojia ya binadamu kwa kumpatia mwanadamu nafasi yake katika kazi ya Uumbaji. Taasisi hii itapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kuheshimu na kuzingatia dhamana na wajibu wa kila taasisi katika ari na moyo wa kushirikiana, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha. Taasisi pia itashirikiana n ana vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazojihusisha na tafiti kuhusiana na maisha ya binadamu!

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.