2016-11-07 15:50:00

Mzee Sitta, Baba wa viwango na mwendo kasi, ameitupa mkono dunia!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora, Mhe. Samwel Sitta. Mhe. Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, 7 Novemba 2016, katika hospitali ya Technical University of Munich, nchini Ujerumani, alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema, amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo. Amesema atamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo, kwa ujasiri wa kusimamia ukweli, tunu alizozionesha kwa kipindi chote alipokuwa kiongozi kwenye ngazi mbalimbali za siasa na serikali.

Rais Magufuli anatoa pole nyingi pia kwa mke wa marehemu Mhe. Magreth Sitta, na familia nzima ya marehemu, kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa wananchi wa Urambo mkoani Tabora, na kwa watu wote walioguswa na msiba huo. Rais Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na anawaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.

Ndugu Samwel Sitta alizaliwa mnamo tarehe 18 Desemba 1942, wilayani Urambo, mkoa wa Tabora. Mbali na kuwa mbunge wa Urambo na baade Spika wa bunge tangu tarehe 26 Desemba 2005 – 16 Julai 2010, ndugu Sitta alikuwa waziri wa mawasiliano na uchukuzi kwa Januari mpaka Novemba 2015, pia Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tangu tarehe 28 Novemba 2010 – 24 Januari 2015.

Ndugu Sitta alihitimu shahada ya sheria mnamo 1971 katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1976 aliamua kujiendeleza, na hivyo kujiunga na chuo kikuu cha IMEDE nchini Uswisi, ambako mwaka huo huo alihitimu stashahada ya juu ya Usimamizi. Alianza mbio za ubunge tangu 1975 - 1995 wakati Jimbo la Urambo halijagawanywa. Wakati wa awamu ya pili ya Rais Mwinyi, ndugu Sitta alikuwa waziri wa katiba na sheria. Ndugu Sitta kafariki leo huko Munich, Ujerumani, akiwa na umri wa miaka 73. Mwenyezi Mungu amrehemu, na ampumzishe kwa amani, Amina

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.