2016-11-07 15:36:00

Mtafuteni na kujitoa kwa Mungu bila ya kujibakiza!


Ni nani awezaye kupanda katika mlima wa Bwana, au nani awezaye kusimama mahali pake patakatifu, ni mwenye mikono safi na moyo mkunjufu, mwenye kuutafuta uso wa Bwana na asiyetamani ubatili (Rej., Zaburi 24). Hao ndio kwa hakika watauona uso wa Bwana. Kwa wimbo huo wa mzaburi, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, na mjumbe maalumu wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Malawi, anawalisha Neno wana wa Mungu, katika adhimisho la Misa Takatifu ndani ya Monasteri ya masista wa Mtakatifu Clara  iliyopo Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi.

Hamu ya kumtafuta na kumuona Mungu katika mazungumzano ya upendo, ni hamu ya wanadamu wote wa kike na wa kiume, ambao huvutwa na tamaa ya kuwa na furaha na ukamilifu, na hivyo kutoridhika mpaka waipate, nayo inapatikana kwa Mungu mwenyewe. Hata hivyo katika hija hii ya kumtafuta Mungu, hayupo mwanadamu anayejitosheleza, bali wote huhitaji wengine kuwaongoza na kuwaonjesha hiyo furaha inayopatikana katika kumtafuta Mungu. Jukumu hili ni la msingi sana kwa wale wanaoishi maisha ya tafakuri, ameeleza Kardinali Filoni.

Changamoto kubwa leo kwa maisha ya wakfu, ni kudumu katika kumtafuta Mungu, na kujitoa kwa Kristo kwa ufukara, usafi wa moyo na utii, ili kuwa kweli ishara hai ya Neno la Mungu, lililofanyika mwili. Kardinali Fernando Filoni, amewakumbusha watawa hao kwamba magumu yapo na changamoto ni kubwa na nyingi, hata hivyo wajifunze kutoka kwa wanafunzi wa Yesu, ambao wanaomba kwa unyenyekevu kuongezewa imani (Rej., Luka 17:5). Sala hii ilikuwa sala ya kina na ya moyo ambayo mababa wa jangwani wa Misri, katika karne za kwanza, waliitumia sana wakiishi maisha ya wakfu. Ilikuwa pia sala ya moyo ya Mt. Francisko na Mt. Klara, ambao kutoka kwao, masista wa Maklara wanapata kujifunza.

Changamoto ya maisha ya jumuiya wataishinda kwa kudumu katika maisha ya kiroho, ukimya na sala, tafakari ya Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho. Kardinali Filoni amewasisitiza masista wa Maklara katika monasteri ya Lilongwe, Malawi kwamba: maisha yao ya jumuiya ni tafakari ya upendo wa Utatu Mtakatifu. Hivyo wawe wema kwa kila mmoja na kusameheana wanapokwazana. Kawahimiza kuendelea kuliombea Kanisa na utume wa walio katika shughuli za kichungaji, wakikumbuka kwamba wao ni kama miji au taa zilizo juu ya vilima. Waangaze na kung’ara ili watu waonje matunda ya sala zao na mifano ya maisha yao.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.