2016-11-07 08:17:00

Mapendekezo ya Vyama vya Kijamii katika maboresho ya maisha ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 5 Novemba 2016, amekutana na wajumbe wa Mkutano mkuu wa tatu wa Shirikisho la Vyama vya Kijamii Kimataifa. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekaza kusema: Jamii inahitaji kuona mabadiliko yatakayowawezesha watu kupata fursa za ajira; wananchi kuweza kumiliki ardhi kwa ajili ya kujipatia chakula na mahitaji yao msingi; watu wanahitaji kuwa na makazi bora na salama. Ubaguzi, nyanyaso, vita na kinzani za kijamii ni mambo ambayo yanadumaza, ustawi na maendeleo ya wengi; Injili ya uhai kwa kukuza na kuendeleza utamaduni wa kifo. Kuna haja sasa ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mshikamano na upendo, ili kuboresha maisha ya watu wengi zaidi pamoja na kuendelea kuwapatia utambulisho wao. Ukoloni mamboleo na utandawazi tenge ni hatari sana kwa maendeleo ya watu.

Wajumbe hao wakitoa mapendekezo ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, myumbo wa uchumi, kinzani za kisiasa na kijamii, wameeleza kwamba, mahangaiko yote ya binadamu leo yanatokana na tamaa ya fedha na kutoheshimu utu wa binadamu. Wamemkumbuka Bertha Caceres, msemaji wa mkutano wao wa kwanza, aliyeuwawa katika harakati za kutafuta mchakato wa mabadiliko, wameomba kusitishwa kwa mateso wanayonyanyaswa wajumbe wa vyama vya kijamii, kwani ni watu wanaotafuta amani iliyojikita katika haki jamii. Kwa upande wa demokrasia kamili na shirikishi, wamependekeza kuhusishwa kwa vyama vya kijamii katika maamuzi msingi ya kisiasa na kiuchumi. Kwa upande wa maliasili, wamedai haki ya nishati ya maji safi kwa kila mmoja, kwani ni haki msingi ya binadamu.

Kuhusu heshima na utu wa watu, wanasisitiza kuheshimu utu wa binadamu katika hatua zote za uhai wake, tangu kutungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida inapomsibu mtu. Zaidi sana, umuhimu wa kupatikana kwa lishe bora na kutokomeza kabisa tatizo la njaa na magonjwa yatokanayo na ukosefu wa lishe. Kwa haki za wafanyakazi, wamependekeza mishahara stahiki kwa wafanyakazi wote na mazingira ya kazi yanayoheshimu utu wa binadamu katika sekta zote. Wameomba pia kuzingatia makazi na maisha bora kwa kila mtu, na kuhesimu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Kwa ujengaji wa madaraja kati ya watu, wameelekeza kilio chao kufutilia mbali ubaguzi wa namna yeyote ile na chuki dhidi ya wageni, hivyo kuzingatia ukarimu wa kuwapokea wahamiaji wote wanaolazimika kuyaacha makazi yao na kukimbilia mahali salama. Mwishoni, wajumbe hawa wameomba kushirikiana bega kwa bega na Baba Mtakatifu Francisko, ili mapendekezo haya yatiliwe maanani na kufanyiwa kazi. Wanaomba Makanisa mahalia kuwa wajumbe waaminifu wa Baba Mtakatifu katika kufanikisha mageuzi ya watu kupata na kumiliki ardhi kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, ajira ili kuwawezesha kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kifamilia na kijamii pamoja na makazi bora kwa watu wote kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ndoto ya Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.