2016-11-07 06:53:00

Jumuiya ya Kimataifa inahitaji utandawazi wa mshikamano


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa katika hotuba yake kuhusu utandawazi na hali ya kutegemeana anasema, kwa asili binadamu ni kiumbe jamii. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mwanadamu bado anakabiliwa na changamoto kubwa katika maisha yake yaani: madhara yanayosababishwa na vitendo vya kigaidi duniani; pengo kubwa la watu ambao hawana uwezo wa kutumia maendeleo haya makubwa ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Kumekuwepo na utengano mkubwa kati ya maendeleo ya viwanda na uchumi wa fedha katika mfumo wa kidigitali, kutoka katika uchumi halisia, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa ubinafsi na ulaji wa kupindukia unaohatarisha mshikamano pamoja na kuendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Taarifa ya mwenendo wa uchumi kimataifa zinaonesha kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimepelekea kudumaa kwa ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea duniani. Kumekuwepo pia ukosefu mkubwa wa fursa za ajira na ongezeko la kiwango cha umaskini wa hali na kipato na kwamba, waathirika wakubwa ni vijana wa kizazi kipya! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika maisha na utume wake, anaendelea kukutana na vijana wanaogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato; tatizo kubwa la kiuchumi linalodhalilisha pia utu na heshima ya binadamu. Pale ambapo hakuna fursa za ajira, uzoefu unaonesha kwamba, si rahisi wazazi kutosheleza mahitaji msingi ya familia zao.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani imefikia million 244. Kuna watu million 40 ambao hawana makazi ya kudumu hata katika nchi zao wenyewe kutokana na kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii. Wakimbizi na wahamiaji hawa wengi wao ni wale wanaotoka katika maeneo ya vita; watu wanaobaguliwa, wanaodhulumiwa, dhalilishwa na kunyanyaswa kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Kuna makundi makubwa ya watu wanaokimbia nchi zao kutokana na umaskini, magonjwa na majanga asilia, ili kutafuta maisha bora zaidi.

Askofu mkuu Auza anasikitika kusema kuwa, wahamiaji na wakimbizi hawa wanapofika kwenye nchi wahisani, wengi wao wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo. Ni makundi ya watu wanaoteseka kutoka na ubaguzi, misimamo mikali ya utaifa na ukosefu wa sera makini za kuwapokea, kuwakaribisha na kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya jamii husika.

Hapa kunakosekana utashi wa utandawazi unaojikita katika msingi wa kutegemezana. Hii ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anaendelea kulihamasisha Kanisa Katoliki pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano kwa kujikita katika utandawazi unaojali na kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Wakimbizi na wahamiaji ni kati ya makundi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Askofu mkuu Auza anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti kikamilifu katika mapambano dhidi ya miundo mbinu inayoendelea kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; umaskini, njaa na magonjwa, sanjari na kulinda mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mambo haya yakidumishwa, utu na heshima ya binadamu vitakuzwa na kuendelezwa, watu watapata fursa za ajira, elimu itaweza kuboreka zaidi na familia kupata ulinzi na tunza ya kutosha kuweza kutekeleza dhamana na majukumu yake katika jamii.

Hizi ni mbinu mkakati za ujenzi wa utandawazi na kutegemezana, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Hapa mataifa hayana budi kuondokana na ubinafsi n autaifa usiokuwa na tija wala mashiko katika medani za kimataifa. Ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kuna haja ya kujikita katika utamaduni wa majadiliano, upendo na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Watu wajenge madaraja ya kukutana na jirani zao, badala ya kujenga kuta za utengano na ubaguzi wa watu mambo ambayo yamepitwa na wakati.  Haya ni mambo nyeti anakaza kusema Baba Mtakatifu, lakini yakizingatiwa na wengi, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo kwa kuzipatia suluhu ya kudumu na katika usawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.