2016-11-06 07:24:00

Umuhimu wa ukimya katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa!


Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Nidhamu na Sakramenti za Kanisa anazungumzia kuhusu umuhimu wa ukimya katika maadhimisho ya Ibada mbali mbali za Kanisa ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kukombolewa. Liturujia inawajenga waamini kuwa kweli ni Hekalu takatifu na Makao ya Mungu katika roho; inawaimarisha waamini kuwa ni mashuhuda wa Kristo kwa maneno na maisha yao adili.  Ukimya ni muhimu sana katika maadhimisho ya Ibada mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee, katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuwasaidia waamini kupyaisha maisha yao, kielelezo makini cha Liturujia ya Kanisa.

Ukimya unapaswa kuchukuliwa katika mwelekeo chanya unaojipambanua kutoka katika ugumu wa mioyo, kiburi na kisirani katika maisha ya mwanadamu. Ukimya unamwezesha mwamini kuvunja kuta na vizingiti vinavyokwamisha mchakato wa kusali vyema, ili kuweza kuungana kikamilifu na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yake. Ni kwa njia ya sala makini, Mwenyezi Mungu anaweza kuongea na waja wake kwa kuwakirimia utajiri wa maisha na uwepo wake endelevu, unaomjaza huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, hapa sala ni kielelezo cha ukimya wa maisha ya kiroho.

Maandiko Matakatifu yanakiri kwamba, Ukimya ni kielelezo cha Ibada na Uchaji wa Mungu unaomwandaa mwamini kushuhudia ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yake. Yale yaliyomo moyoni mwa mwanadamu ndiyo yanayomtia unajisi. Yesu anasema, moyoni mwa mwanadamu hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wivu, ushuhuda wa uongo na matusi. Ukimya ni utamaduni unaotoa nafasi kwa wengine, lakini kwa namna ya pekee kwa Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo alivyofanya Bikira Maria mbele ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo.

Ukimya ni tunu inayomwezesha mwamini kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yake, kwa kutambua kwamba, Mungu anatenda kwa njia ya Neno wake aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwamini katika maisha yake, anaendeleza kazi ya Ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu. Waamini wajitahidi kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuzungumza nao! Nambari za simu za mioyo yao, ziwe wazi, tayari kusikiliza sauti ya Mungu inayozungumza nao kwa njia ya dhamiri nyofu. Wawe tayari kuanzisha mchakato wa mazungumzo na Mungu, kwa kumwachia Mungu nafasi katika maisha na vipaumbele vyao.

Kardinali Sarah anasema, waamini wawe na ujasiri wa kumwachia Mungu nafasi ya kusafisha na kuunda akili na nyoyo zao, ili waweze daima kujitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, jambo ambalo ni kitendawili kikubwa kwa waamini. Sala ni majadiliano na mazungumzo na Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, ni sehemu muhimu sana katika Liturujia ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanawaalika waamini kwa namna ya peke kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada mbali mbali kwa kushangilia, kuitikia, kuimba na unyamavu mtakatifu utumike wakati unapodaiwa. Dhana ya ukimya imepewa kipaumbele cha pekee pia na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika Liturujia ya Kanisa.

Kardinali Sarah anakaza kusema, busara itumike kwa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, Nyumba ya Mungu haigeuzwi kuwa ni mahali pa mikutano na utambulisho wa wanasiasa au watu mashuhuri ndani ya jamii. Ibada inayoadhimishwa vyema haina budi kuwa na kipindi pia cha ukimya unaojikita katika undani pia wa moyo na akili ya binadamu, ili kuzamisha Neno la Mungu baada ya tafakari, na kumshukuru Kristo baada ya Komunyo. Ukimya si kipindi cha kupiga miayo au kuchapa usingizi Kanisani!

Ukimya ni sehemu ya Liturujia ya Kanisa unaomwezesha mwamini kupata utulivu na amani ya ndani na wala si wakati wa kumangisha mangisha mawazo! Hii ni fursa ya kumwachia Mungu aweze kuwagusa waamini kwa njia ya upendo wake. Wakati wa matoleo, inafaa kukaa kimya kidogo, ili kujiandaa kwa matoleo, ili mwamini aweze kuunganisha maisha yake na sadaka ya Kristo inayotolewa Altareni. Hapa Kardinali Sarah anasema, kwa baadhi ya Makanisa Barani Afrika hapa ndipo mahali pa waamini kujimwaga kwa nyimbo na midundo moto moto; kwa maandamano marefu yanayokwenda wakati mwingine kama kinyonga!

Pengine umefika wakati wa kufanya tafakari ya kina kwa umakini mkubwa, ili kutambua kwamba, matoleo ya waamini yanapaswa kuunganishwa na Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo linaloadhimishwa wakati huo Altareni. Ukimya huu unaweza kuwa ni ushiriki mkamilifu wa waamini katika sadaka ya Kristo Msalabani, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa njia hii, anasema Kardinali Robert Sarah katika tafakari yake juu ya umuhimu wa Ukimya katika Ibada mbali mbali za Kanisa unaweza kupata maana kamili katika maisha ya waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.