2016-11-05 16:20:00

Yesu analichambua Fumbo la Kifo kama karanga!


Kumepita karibu miaka laki moja na nusu kutoka alipovuvumka binadamu na kujikuta anayo akili ya kujitambua wenyewe na anao utashi wa kuchagua. Kwa njia ya akili na utashi huo binadamu daima amejihoji ametoka wapi, yuko wapi na hatima yake ni ipi. Swali  nyeti zaidi linalosononesha moyo wa binadamu ni pale anapofikiria hatima ya maisha yake yaani kifo. Kwa nini maisha yake yanakoma pindi yeye anataka bado kuishi. Binadamu amefurukuta kulifumbua fumbo hilo lakini hakufika popote. Hebu tuyafuatilie majibu mbalimbali aliyojaribu kuyatoa binadamu katika maisha.

Wamisri ni taifa mojawapo lililojaribu kujibu swali hilo. Wao walihifadhi maiti ili yasioze wakayaita Mumiani. Lengo lilikuwa ni kukisimanga kifo kwamba hata kama kimemchukua mpendwa wao bado wanaweza kumhifadhi mfu huyo na kuendelea kukaa naye. Kwa hiyo kifo kimekula kwake. Lakini wasijue kwa kufanya hivyo walikuwa wanakienzi tu kifo kwa kukijengea makumbusho au sanamu. Wasumeri na Wamesopotamia walijiuliza maswali ya kifo na majibu waliyopata katika fasihi na mithiolojia zao ni kwamba mtu akiacha ulimwengu huu anaenda katika ulimwengu ambao hawezi tena kurudi duniani. Lakini hawakujua ni wapi anaenda.

Wagiriki walijibu swali hilo katika mithiolojia ya mwanamuziki Orfeo. Huyo Orfeo alikuwa akipiga muziki wake wa kinubi alivuta kila kiumbe kuanzia milima, mawe, miti, wanyama, ndege kuja kumsikiliza na hata kucheza muziki aliokuwa anaupiga. Lakini Orfeo mwenyewe baadaye alikufa akashindwa kabisa kukitawala kifo. Mithiolojia hiyo inataka kutuambia kwamba hapa duniani binadamu anaweza kutumia ufundi wake wote kuvuta na kutawala akili na vionjo vya watu hata viumbe vingine vyote, lakini hawezi kukitawala kifo. Kadhalika magwiji wa filosofia kama Sokrates, Aristotle, nao walishindwa kabisa kujibu kiyakinifu swali hilo nyeti la kifo, kwani walijua kwamba hatima yao ni kaburi.

Mwafrika haoni suala la kifo kuwa ni swali la kujitaabisha kujibu. Yeye anajua jambo moja tu kwamba Mungu mwumbaji ndiye aliyetuleta hapa duniani, na tunapokufa tunaenda kujiunga naye pamoja na mahoka waliotutangulia. Kwa hiyo marehemu wanarudi nyumbani walikotoka. Wayahudi (Israeli) wao waliamini kwamba baada ya kufa, watu wote tunaishia kuzimu yaani Sheol au Shaal maana yake ni kuita. Sheol kuna mizimu, na maisha yake hayana maana  kwani  huko huwezi kumsifu Mungu. Kwa hiyo hata baba wa imani Abrahamu hadi manabii wote kama Yeremia na Isaya, na mfalme Daudi, wangeulizwa kama wanaelewa chochote kinachomtokea binadamu baada ya kufa wasingekuwa na jibu. Walichofahamu wao ni kumwabudu Mungu ili awaongoze wawe na furaha hapa ulimwenguni. Kwa vyovyote watu hawa wametufundisha jinsi gani yabidi kuyapatia umuhimu maisha ya ulimwengu huu.

Wazo la ufufuko kwa Waisraeli linatokea kwa mara ya kwanza katika Kitabu cha Danieli kilichoandikwa miaka mia moja na sabini hivi yaani nusu ya pili ya karne ya pili kabla ya Kristu. Wayahudi wa karne hiyo  hasahasa wakati wa madhulumu ya Waseleuchi, wakaanza kuzungumzia juu ya mashahidi na wenye haki. Wakajiuliza hatima ya wenye haki, waaminifu kwa Torah, ile wa waovu na wadhulumu waliotaka kufifisha mapokeo ya kidini ya wayahudi itakuwaje pale atakapofika Masiha na kuingiza ulimwengu mpya? Jibu likawa kwamba hao wenye haki na mashahidi wataibuka kutoka kwenye makaburi ili kushiriki furaha ya ufalme na utawala wa Mungu yaani watafufuka na waovu watasota huko huko makaburini. Wenye haki peke yao ndiyo watafufuka na kuishi tena maisha haya haya. Hivi ndivyo alivyojua Marta alipomjibu Yesu: “Mimi ninajua kwamba kaka yangu Lazaro atafufuka siku ya mwisho.”

Wazaburi, wakalijibu swali la hatima ya binadamu kwa njia ya tenzi na zaburi za kumsifu Mungu. Wazaburi walimpenda sana Mungu na waliwasiliana naye katika sala na walijisikia wao kuwa ni hasid wa Mungu. Kwa hiyo waliamini kwamba wapendanao wataungana pamoja kama anavyosema mzaburi mwenyewe: “Maana hutaacha roho yangu kuzimu, wala hutamwonesha uharibifu anayekuaminia. Utanionesha njia ya uzima, utanipa shibe na furaha, kuume kwako nitastarehe milele.” (Zab 16:10-11). Hata hivyo, fikra hizo za mzaburi hazikuwa za uhakika na za kuthibitika juu ya maisha baada ya kifo.

Katika Injili ya leo tunakutana na Wasadukayo wasiosadiki kabisa juu ya ufufuko. Jina hili Sadukayo linatokana na Kuhani mkuu Sadok aliyeishi wakati wa mfalme Sulemani. Baadaye wafuasi wake wakajulikana katika utawala wa warumi na walipewa hadhi ya juu sana. Kikundi hiki cha Wasadukayo kilisambaratika mwaka wa sabini lilipobomolewa hekalu la Yerusalemu. Katika Injili kumebaki majina mawili tu yanayowataja Wasadukayo yaani Anna na Kaifa waliohusika na kifo cha Yesu. Wasadukayo walijisikia kuwa ni washenga kati ya Mungu na watu. Sadaka na baraka zote zilipitia kwao.

Walikuwa na msimamo mkali wa dini na wa kufuatilia kwa dhati madhehebu ya hekaluni. Masuala ya pesa na uchumi vyote vilikuwa chini yao, hivi wakawa matajiri kupindukia walioisharidhika na maisha. Wasadukayo walitoa sadaka na kumwomba Mungu ili awabariki kusudi waendelee kuwa matajiri na kuishi vizuri hapa duniani kwani walijua baada ya kifo watu waliishia katika sheol. Kwa hiyo mahusiano yao na Mungu yalilala katika uchumi, ndiyo maana Yesu alipoingia hekaluni alizipinduana meza za kubadilishia fedha. Wasadukayo, walijua kwamba Yesu alikuwa anafikiri kama Wafarisayo yaani Wayahudi wengine. Hivi wakamwendea na kumwuliza swali juu ya ufufuko kama wanavyojua Waisraeli wote.

Wasadukayo wakaliwakilisha suala la mwanamke yule aliyekuwa na wanaume saba. Wanamwuliza Yesu kuwa, kama ufufuko ni kurudi tena katika maisha haya ya kibaolojia ya kuoa na kuoana, hapo kadiri ya sheria zilizowaruhusu ndugu kuridhishana lipwela, siku ya ufufuo kutakuwa na sokomoko la kugombanea mwanamke aliyeolewa na wanaume saba. Yesu akawajibu: “Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa, lakini wale wanaoingia katika ufalme wa Mungu ujayo, hao wako katika ufufuko wa wafu, hao ni kama malaika, hawaoi wala kuolewa.”

Maisha hayo ni tofauti kabisa na maisha ya kibaolojia kwani ni maisha ya upendo. Katika ufufuko Yesu harudi tena ulimwenguni na mwili wa utukufu wa kibinadamu, bali anaenda Sheol na mwili wa utukufu ili kuwahamisha wafu wote na kwenda nao katika ulimwengu wa Mungu. Ndiyo maana katika Injili ya Marko, siku ya ufufuko wa Yesu wamama wanapofika kaburini wanakutana na kijana, anayewaambia: “Yesu aliyesulibiwa hayuko hapa, na siyo yeye bali hakuna kilichobaki hapa, kwani yeye na waliokuwa hapa wameenda maisha mengine. Wameingia katika ulimwengu wa milele wa Mungu.” Hapa Yesu anatupatia kwanza maana ya maisha haya, halafu anatoa hatima ya maisha haya kuwa ni maandalizi ya maisha ya milele ambayo tutayaishi katika ulimwengu wa Mungu.

Sehemu ya pili ya Injili ni muhimu sana, kwani Yesu anarejea kwenye ulimwengu wa kibiblia, ambapo wengi wanafufuka na kuingia katika ulimwengu wa Mungu. Hivi ananukuu kitabu cha Kutoka sura ya tatu. Anaonesha kwamba huyo ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaaki na Mungu wa Yakobo. Watu wa kale walikuwa wa miungu wa mahala, waliohusiana na watu fulani, mathalani mungu Benadadi wa Damasko-Siriani; mungu Merka wa Ramatamoni yaani wamoniti; mungu Amoni wa Wamisri. Kadhalika Uyahudini kulikuwa na mungu wa sichemu, mungu wa Betel, mungu wa Aman  nk. Kumbe Mungu anayetajwa hapa siyo mungu aliyejikita pahala fulani, la hasha bali ni Mungu wa binadamu.

Kwa hiyo kama Mungu huyo ni binadamu Abraham, Isaak na Yakobo, hao hawatakufa. Kama hao wanakufa na kufifia, basi Mungu wao atakuwa ni wa wafu. Lakini kama ni Mungu wa wazima basi huyo hawezi kuwaacha marafiki (mahasid) na waswahibu wake wabaki kaburini. Kwa hiyo “Kama Mungu yuko basi sitakufa.” Hivi jibu la uhakika  la hatima ya binadamu limedhihirika katika ufufuko wa Yesu. Katika Kristu, uzima wa kweli na wa milele umeingia katika mwili huu unaokufa.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB. 








All the contents on this site are copyrighted ©.