2016-11-05 11:49:00

Washirikisheni maskini kujadili hatima na mustakabali wa maisha yao


Mkutano mkuu wa tatu wa wanaharakati wa maendeleo kimataifa ulioanza hapo tarehe 2 – 5 Novemba, 2016 imekuwa ni fursa ya kujadili mambo msingi yanayohitajika kwa ajili ya kusukuma mbele mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu; yanayojikita kwa namna ya pekee katika mambo makuu matatu: Ardhi, Makazi na Ajira. Haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko amekuwa pia akiyapatia kipaumbele cha pekee, anasema, Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican. Mkutano huu umeandaliwa na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kuwashirikisha wajumbe zaidi ya mia mbili kutoka katika nchi 62 duniani.

Wanasiasa na watunga sera katika Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuhakikisha kwamba, watu wote wanahusishwa katika mchakato wa maendeleo endelevu, ili kupambana na umaskini wa hali na kipato; jambo linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake vinapewa kipaumbele cha kwanza bila kuwasahau watu wanaoishi pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amekuwa akiunga mkono juhudi za wanahakari wa kimataifa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya watu, kwa kukazia: Ardhi, Makazi na Ajira. Hii ni sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa sanjari na utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji inapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuonesha upendo na mshikamano. Wajumbe wa mkutano huu wa kimataifa wameangalia kwa makini changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Sehemu ya pili wakaamua ni mambo yepi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na tatu; utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa katika mkutano huu. Wanachama wa harakati za maendeleo kimataifa wanasema, hakuna sababu msingi ya kukata tamaa katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato duniani, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashikamana na kuongozwa na kanuni auni kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kuwa ni wadau wakuu wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kwamba, wanapata fursa ya kumiliki ardhi kama rasilimali katika mchakato wa maboresho ya maisha; wanakuwa na makazi bora, safi na salama ili kulinda na kudumisha afya bora na tatu wanapata fursa ya ajira, ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Haya ni mambo msingi katika mageuzi ya sekta ya kilimo pamoja utunzaji bora wa mazingira anasema Bwana Juan Grabois, mshauri, Baraza la Kipapa la haki na amani. Wajumbe wa mkutano huu, pamoja na mambo mengine, wameangalia jinsi ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo ni kutoa huduma bora kwa wakimbizi na wahamiaji; kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwenye maeneo ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Kwa upande wake, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, Kanisa linapenda kuunganisha sauti yake na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuwa ni wadau wa mageuzi ya kijamii kwa kusimama kidete kupambana na uchu wa mali na madaraka sanjari na ukosefu wa haki jamii. Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari kwa kuwajengea uwezo maskini, ili waweze kuboresha maisha yao kwa kutumia rasilimali iliyopo.

Maskini duniani wanapaswa kuungana na kushikamana, ilikujadili hatima na mustakabali wa maisha yao. Kilio cha maskini na watu wasiokuwa na sauti ndicho kinacholiwajibisha Kanisa kusimama kidete, ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wa nyakati hizi anasema Kardinali Peter Turkson. Kanisa linataka kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema kupambana na umaskini duniani. Kanisa na wanaharakati wa maendeleo endelevu wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Haki za wafanyakazi na wanawake zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.