2016-11-05 15:19:00

Wasaidieni watu kujenga matumaini kwa siku za usoni!


Baba Mtakatifu Francisko, kupitia kwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ametuma ujumbe Baraza la Maaskofu Katoliki wa Ufaransa, akionesha furaha ya kushiriki pamoja nao kwa sala na ukaribu wa kiroho, ambapo maaskofu hao wanafanya mkutano wao mkuu wa mwaka, huko Lourdes, Ufaransa. Wakati wakiwa bado katika mazingira ya matishio ya ugaidi na harakati za kufanya uchaguzi mkuu nchini mwao, Baba Mtakatifu Francisko anawatia moyo maaskofu wa Ufaransa kuwasaidia wakazi wote nchini humo, wadumu katika matumaini na kushiriki kwa pamoja kutafuta mafao ya wengi. Wataweza kufanya hivyo kwa kupitia utume wao wa kikuhani, wanapokuwa wakidhihirisha utendaji wa kichungaji, hasa kwa kuwasaidia mapadri vijana kuupyaisha kila siku wito wao wa utume na kuutimiza kwa furaha.

Anawaalika kutafakari kwa kina juu ya kuwa wajasiri kiutendaji, ili kuwafikia wote walio pembezoni na wanaohitaji kuinjilishwa, na kwa namna hiyo kuweza kuona nafasi ya kueneza Injili kwa kina, kupitia sehemu zinazoendelea kubadilika, zilizoko pembeni mwa miji. Kanisa linapoelekea kuadhimisha kilele cha mwaka wa huruma, katika siku kuu ya Kristo Mfalme, 20 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika maaskofu wa ufaransa, kuwasaidia waaamini wote nchini humo, kuitazama miaka ya usoni, kuwa ni miaka ya kuzama zaidi katika huruma, katika kukutana na Mungu mwema na mwenye upole.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.