2016-11-05 16:01:00

Bado kuna ubaguzi wa rangi na hali ya kutovumiliana duniani!


Mwaka 2015, Umoja wa Mataifa uliadhimisha miaka 50 ya harakati za utokomezaji wa aina zote za ubaguzi wa watu. Hata hivyo katika miaka hii ya karibuni, dunia imeshuhudia wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi sehemu mbali mbali, jambo ambalo limedhihirisha kwamba, bado sehemu nyingi duniani kuna hisia za ubaguzi wa rangi, unyanyapaaji na chuki kwa wageni. Ndivyo Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, anavyofungua hotuba yake juu ya ubaguzi na chuki kwa wageni, katika Mkutano wa Umoja huo Jijini New York. Kamati ya Haki msingi za binadamu katika Umoja huo, imeanisha hivi karibuni hatari ya makundi na vyama vya siasa kali sehemu nyingi duniani, wanavyodhoofisha harakati za upatikanaji amani duniani, na ujengwaji wa haki jamii zinazokumbatia watu wa makabila, rangi na mataifa yote, kufikia mwaka 2030.

Taarifa zinaonesha kwamba, kumekuwa na ongezeko kubwa la chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa watu kimataifa, ikiwa ni pamoja na machafuko na mapigano. Askofu Mkuu Auza anatahadharisha kwamba, inaonekana siasa za leo katika sehemu nyingi, zinaendeshwa kwa hofu, hofu ya jirani au mgeni au mtu mwenye mtazamo tofauti. Hofu ya kuwajibika na kuwahangaikia wanyonge na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, hofu ya kuwajali wahitaji na wanaohitaji mshikamano na huruma. Inasikitisha kuona kwamba mpaka sasa kwa mwaka huu 2016, idadi ya wahamiaji waliofariki katika harakati za kuvuka bahari ya Mediterania  imeishafikia 3,740.

Utu wa mwanadamu hauamuliwi na sheria za nchi, awe raia au mgeni, utu wa binadamu sio suala la kujiuliza mara mbili au kutafutia maridhiano kwa mazungumzano, ni suala la kuuheshimu na kuulinda. Kama Baba Mtakatifu Francisko anavyosema: wahamiaji wasitazamwe katika hali zao za kuwa mahali fulani kisheria au la, bali watazamwe kwanza kabisa kwamba ni wanadamu wenye utu unaopaswa kulindwa na wenye uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya jamii wanamojikuta. Hili linawezekana ambapo wanaowapokea, nchi wenyeji, watafanya hivyo kwa ukarimu, heshima na kuwapa nafasi za kushiriki maisha ya kawaida ya mahali hapo. Askofu mkuu Auza, kawaalika Jumiya ya Kimataifa, kuzingatia kwa makini na kupambana kwa pamoja ili kutokomeza ubaguzi wa kila aina, na kuthamini utu wa mtu, hasa wakati huu wa wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.   

 








All the contents on this site are copyrighted ©.