2016-11-04 15:33:00

Shuhudieni imani yenu na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira!


Ubatizo, Ekarissti Takatifu na Kipaimara ni Sakramenti zinazomwingiza mwamini katika Ukristo na kukamilisha neema ya Ubatizo. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu hivyo hulazimika kwa nguvu zaidi kuishuhudia, kuieneza na kuitetea imani yao kwa maneno, lakini zaidi kwa njia matendo kama mashuhuda amini na wa kweli wa Kristo!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 70 kwenye Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu, Eneo la Kisasa, Jimbo kuu la Dodoma. Askofu mkuu Kinyaiya aliwataka waamini kuwa ni mashuhuda wa imani yao inayomwilishwa katika matendo. Amewataka waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Habari Njema ya Wokovu; huruma na upendo wa Mungu unaowaambata wote pasi na ubaguzi.

Lakini kwa namna ya pekee, wawe mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kanuni maadili na utu wema. Lengo ni kuweza kujipatia mkate wa kila siku kwa njia halali na kamwe wasitafute njia ya mkato! Wajitahidi kujenga urafiki na Mungu kwa matendo ya huruma na mapendo, ili kupata amani na utulivu wa ndani, kama ilivyokuwa kwa Zakayo Mtoza ushuru aliyeonja huruma ya Mungu, akatubu na kumwongokea Mungu kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa maskini!

Waamini waoneshe moyo wa ukarimu na kuachana na ubinafsi unaoweza kuwatumbukiza katika uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni majanga ya kijamii. Vijana wanapenda kupata utajiri wa chapu chapu anasikitika kusema Askofu mkuu Kinyaiya na hali hii si sahihi na kwamba, vijana wajenge utamaduni wa kujipatia kipato chao kwa njia halali ili kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema katika maisha, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika maadili na utu wema.

Hii inatokana na ukweli kwamba, uchafuzi wa mazingira umekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Watanzania wasipokuwa makini, wakajikita katika mchakato wa maboresho ya mazingira, nchi itageuka kuwa ni jangwa na mahali ambapo hapafai kwa maisha ya mwanadamu! Kumekuwepo na ukataji mkubwa wa miti kwa ajili ya kupata kuni na mkaa, mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira nchini Tanzania.

Umefika wakati kwa Serikali ya Tanzania kuhamasisha matumizi ya gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani kama sehemu ya mkakati wa kulina na kutunza mazingira dhidi ya uharibifu wa mazingira kwa kutafuta kuni na mkaa. Askofu mkuu Kinyaiya amewataka wazazi na walezi wawe mfano bora wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo wanamoishi na kufanya kazi, ili kweli Mji wa Dodoma unaoendelea kukua kwa mwendo mdundo, uweze kuwa ni mahali penye mvuto na mashiko kwa watu wanaohamia mjini humo kutokana na uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli kuhakikisha kwamba, Makao makuu ya Serikali yanahamia Dodoma kama sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyoitoa takribaini miaka 50 iliyopita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.