2016-11-04 07:47:00

Kumekucha! Hakuna mtu anayetengwa na huruma ya Mungu!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 6 Novemba 2016 utapambwa kwa uwepo na ushiriki wa wafungwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafungwa. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, Alhamisi 3 Novemba 2016 wakati akiwasilisha yale yatakayojiri wakati wa Jubilei ya wafungwa. Askofu mkuu Fisichella anafafanua kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya wafungwa yanaonesha kwa namna ya pekee, jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anavyotoa kipaumbele cha pekee kwa wafungwa

.

Mara nyingi Baba Mtakatifu wakati wa hija zake za kitume, amependa kutembelea, kusali na kuzungumza na wafungwa, ili kuwaonjesha pia huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kumwokoa mwanadamu, ili aweze kugeuka na kuwa mtu mpya zaidi. Baba Mtakatifu anafanya yote haya kuwaonesha na kuwaonjesha wafungwa uwepo wake wa kibaba kwa njia ya sala katika shida na mahangaiko yao ya ndani, ili waweze kuwa na matumaini mapya katika maisha yao kwa siku za baadaye. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu aliweza kuzungumza kwa njia ya simu na mfungwa ambaye anasubiri adhabu ya kifo huko Marekani.

Kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei hii, wafungwa pamoja na familia zao, Askari magereza pamoja na viongozi wa magereza watapata nafasi ya kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya wafungwa, bila kuvisahau vyama mbali mbali vya kitume vinavyojisadaka kwa ajili ya huduma kwa watuhumiwa na wafungwa magerezani. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 4, 000 watashiriki katika tukio hili la kihistoria. Zaidi ya wafungwa elfu moja kutoka katika majimbo kumi na mawili duniani wanashiriki.

Hawa ni wafungwa kutoka: Uingereza, Italia, Lithuania, Madagascar, Malaysia, Mexico, Ireland, Hispania, Marekani, Afrika ya Kusini pamoja na wajumbe wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kutoka Sweden. Itakumbukwa kwamba, ni hivi karibuni tu, Baba Mtakatifu Francisko amerejea kutoka kwenye hija yake ya kitume nchini Sweden alikokuwa anashiriki matukio ya kiekumene na kikanisa! Kutakuwepo na uwakilishi wa makundi ya wafungwa: Watoto watukutu; wafungwa wanaotumikia adhabu ya nje; wafungwa walioko kizuizini pamoja na wafungwa waliokwisha hukumiwa!

Askofu mkuu Fisichella anapenda kuishukuru Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi ya Italia kwa kuonesha ushirikiano na mshikamano, kiasi hata cha kuwezesha wafungwa sita kutoka katika magereza ya Italia, kushiriki katika huduma za kujitolea wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, itaanza majira ya saa 4: 00 kwa saa za Ulaya. Kabla ya maadhimisho haya, waamini wataweza kusikiliza shuhuda za wafungwa wanne. Mmoja atashuhudia kuhusu toba na wongofu wa ndani alioupata na msamaha uliotolewa na mtu aliyemtendea kosa hili.

Shuhuda mwingine atazungumzia uponyaji wa ndani, huruma na msamaha walioonesha baada ya kaka yao kuuwawa kikatili. Kijana anayetumikia kifungo kwenye gereza la watoto watukutu atapata naye nafasi ya kushirikisha machungu ya maisha anayopambana nayo huko gerezani lakini akiwa na mwanga wa Injili. Mwishoni, Askari magereza ambaye maisha na utume wake uko gerezani kila siku, atashuhudia changamoto wanazokabiliana nazo. Shuhuda hizi zitakuwa zinasindikizwa kwa muziki utakaocharazwa kwa ufundi mkubwa na wafungwa kutoka Gereza la Dozza, Bologna, nchini Italia. Wasimamizi na watumishi wa Liturujia hii, watakuwa ni wafungwa wenyewe, matendo makuu ya Mungu anayemwonesha mwanadamu Uso wa huruma, ili aweze kutubu na kumwongokea tena! Hostia zitakazotumika wakati wa Ibada ya Misa takatifu ni zile ambazo zimetengenezwa na wafungwa gerezani.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, kati ya tarehe 11- 13 Novemba, 2016 kutakuwa na maadhimisho ya Jubilei kwa ajili maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali katika maisha. Baadhi yao ni wale ambao wameathirika kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa; wagonjwa; wapweke na wale ambao wametengwa na familia zao kutokana na sababu mbali mbali. Wengine ni wale ambao hawana makazi wala mahali pa kulaza vichwa vyao. Barabara za mijini ndiko wanakopata hifadhi ya maisha yao.

Zaidi ya watu elfu sita kutoka: Ufaransa, Ujerumani, Ureno, Uingereza, Hispania, Poland, Ireland, Italia, Hungaria, Slovacchia, Croatia na Uswiss watashiriki kikamilifu. Tukio hili limeandaliwa na Shirikisho la vyama vya kitume kutoka Ufaransa vinavyowahudumia maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Shirikisho lililoanzishwa na  E’tienne Villemain. Shirikisho hili limejitwika dhamana na jukumu ya kuhamasisha na kuratibu maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu mkuu Fisichella anakumbusha kwamba, Jumapili tarehe 13 Novemba 2016, Makanisa yote mahalia na madhabahu ya Malango ya huruma ya Mungu, yatafungwa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko, atafunga Lango la huruma ya Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, hapo tarehe 20 Novemba 2016, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Tukio hili litatanguliwa na Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya, walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 19 Novemba 2016. Taarifa zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe 30 Oktoba 2016, idadi ya mahujaji waliohudhuria kwenye Ibada za maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu mjini Roma, ilikuwa imegota millioni ishirini na usheeee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.