2016-11-04 14:29:00

Kanisa linawakumbuka Maaskofu kwa ushuhuda wa Kikristo na Kipadre


Bwana amejaa huruma na neema, ndiyo maana Mwezi Novemba, Mama Kanisa anautolea maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watoto wake waliolala kwenye usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu; ili hatimaye, waweze kuonana na Kristo Yesu, ili kuishi naye milele yote! Yesu ni hakimu mwenye haki atawahukumu walimwengu kwa kutumia kigezo cha huruma na neema.

Kwa kutambua huruma ya Mungu, Ijumaa, tarehe 4 Novemba, 2016, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha mwaka 2015- 2016. Baba Mtakatifu amewaweka viongozi hawa wa Kanisa chini ya wema na huruma ya Mungu, kwa kutambua ushuhuda wao wa Kikristo na Kipadre ambao wameliachia Kanisa la Kristo!

Viongozi hawa wa Kanisa wamefikia hatima ya maisha yao baada ya kulitumikia Kanisa na kumpenda Kristo Yesu na kwamba, kwa sasa hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenganisha na upendo wa Kristo! Si shida, dhiki wala adha; upanga au hatari ya maisha. Waamini katika upendo wanabaki wakiwa wameungana na Mwenyezi Mungu, ili kufurahia maisha ya uzima wa milele, amani na utulivu nyumbani kwa Baba. Yesu Kristo ndiye anayewaongoza wafuasi wake kwenda kwa Baba wa milele kwani Yeye ni njia, ukweli na uzima!

Baba Mtakatifu Francisko analifafanua Fumbo la kifo katika maisha ya mwanadamu kwa kusema kwamba, hija hii kuelekea nyumbani kwa Baba wa milele inaanza tangu pale mtu anapozaliwa na kufungua macho yake hapa duniani; anapopata neema kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Lakini hatua hii ni muhimu sana kwa Wakleri pale wanapotikia kwa sauti kuu kwa kusema, “Mimi hapa”, siku ile wanapopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, Mapadre wanakuwa wameungana na Kristo kwa namna ya pekee kabisa, kwa kushirikishwa Ukuhani wa Kristo katika huduma.

Wakati wa kuitupa mkono dunia, wanasema tena “Mimi hapa”, huku wakiwa wameungana na Kristo Yesu aliyefariki dunia akiiweka roho yake mikononi mwa Baba wa milele. Makardinali na Maaskofu ambao wamekumbukwa katika Ibada hii ya Misa Takatifu katika maisha yao yote, lakini zaidi mara baada ya kuwekwa wakfu kwa Mungu, wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushuhudia na kujimega kwa ajili wengine kwa njia ya upendo wa Kristo. Kwa njia ya ushuhuda wa maneno na maisha yao adili na matakatifu, wakawahamasisha waamini wengine kufanya vile vile!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hawa walikuwa ni Wachungaji wa Kondoo wa Kristo na kwa kumuiga Kristo, walijimega, wakajisadaka na kujitoa kimasomaso kwa ajili ya wokovu wa familia ya Mungu iliyokuwa imekabidhiwa kwao. Wamewatakatifuza kwa njia ya Sakramenti za Kanisa; wakawaongoza kwenye njia ya uzima wa milele; huku wakiwa wamejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu wametangaza na kushuhudia Injili. Kwa njia ya upendo wa kibaba wamejitahidi kuwapenda wote pasi na ubaguzi, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wanyonge na wahiatji zaidi.

Baada ya maisha yao ya hapa duniani, Kanisa linatumaini kwamba, Kristo Yesu ataifurahia sadaka yao. Kanisa linamtolea Mwenyezi Mungu Sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, ili waweze kung’ara daima katika Ufalme wa mwanga. Kwa njia ya huduma yao ya Kikuhani wameacha chapa ya kudumu katika nyoyo za watu ukweli unaofariji kwamba neema na huruma ni kwa ajili ya wamchao. Kwa jina la Mungu mwingi wa huruma, mapendo na msamaha; mikono yao imeweza kubariki na kuwaondolea watu dhambi zao! Maneno yao yamewafariji na kuwapangusa watu machozi! Ushuhuda wao amini wametangaza wema na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, baadhi yao wamekuwa ni mashuhuda shujaa wa Injili, kiasi hata cha kuvumilia mateso na mahangaiko makubwa. Katika Ibada ya Misa Takatifu, kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa kwa wema na ukarimu aliolitendea Kanisa lake kwa njia ya ndugu na mababa hawa katika imani.

Katika mwanga wa Fumbo la Pasaka ya Kristo, kifo chao ni tiketi ya kuwaingiza katika utumilifu wa maisha. Kwa njia ya mwanga huu wa imani, waamini wanaendelea kujisikia kuwa karibu zaidi na ndugu zao marehemu. Ni kweli kwamba, wametenganishwa kwa njia ya kifo, lakini nguvu ya Kristo na Roho wake Mtakatifu anawanganisha kwa undani zaidi. Waamini wataendelea kujisikia kuwa wako karibu nao katika umoja wa watakatifu. Kwa kulishwa na Mkate wa maisha, waamini pamoja na wale waliowatangalia, wanasubiri kwa hamu kubwa siku watakaponana ana kwa ana na Uso angavu wa Baba wa milele. Bikira Maria anaendelea kuwaombea kama anavyowaombea waamini ambao bado wako hapa duniani wakisafiri kwenda nyumbani kwa Baba wa milele; awasaidie ili kamwe wasitengewe na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.