2016-11-03 07:43:00

Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote: Huzuni na Matumaini!


Mbele ya kifo, fumbo la hali ya kibinadamu linakuwa kubwa sana. Kwa namna moja kifo cha mwili ni kawaida, lakini kwa imani kwa kweli kifo ni mshahara wa dhambi. Kwa wale wanaokufa katika neema ya Kristo, kifo ni ushirika katika kifo cha Bwana, ili kuweza pia kushiriki pia ufufuko wake. Kifo ni mwisho wa maisha ya hapa duniani, kwani maisha ya binadamu yanapimwa kwa wakati.

Waamini wanakumbushwa kwamba, mwili ni kiini cha wokovu unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa fumbo la kifo, roho hujitenga na mwili, lakini katika ufufuko Mwenyezi Mungu humrudishia mwanadamu uzima wa milele; kwa mwili uliogeuzwa na kuungana na roho. Kanisa linasadiki na kufundisha juu ya ufufuko wa wafu na uzima wa milele.Kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea waamini marehemu wote waliolala kwenye usingizi wa amani wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 2 Novemba 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye  Makaburi ya “Prima Porta” yaliyoko hapa mjini Roma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake alijikita zaidi kwenye kitabu cha Ayubu ambaye alikuwa anatembea katika giza huku akikaribia mlango wa mauti. Ayubu alikuwa na mateso makali sana moyoni mwake, lakini katika yote, hatimaye, anatangaza ukuu wa Mungu kwa kuonesha  matumaini kwa Mwenyezi Mungu, mtetezi wake ambaye daima yu hai, hatimaye, atasimama juu ya nchi na atafanikiwa kumwona tena!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu kwa upande mmoja inagubikwa na huzuni na kwamba, makaburini ni mahali ambapo panaonesha huzuni ya moyo. Ni mahali ambapo waamini wanawakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa na marafiki wao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu. Makaburi yanawakumbusha waamini kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu.

Baba Mtakatifu anasema, kumbu kumbu ya waamini Marehemu ni tukio la matumaini katika ufufuko wa wafu, ndiyo maana waamini wanaendelea kuyapamba makaburi kwa maua. Ni kumbu kumbu ambayo imechanganyika kati ya huzuni na matumaini; mambo msingi yanayogubika nyoyo za waamini wanapowakumbuka Marehemu wao. Matumaini ya ufufuko wa wafu yanawasaidia waamini kuendelea na hija kuelekea katika Fumbo la kifo, hapa kila mtu anashiriki “kivyake vyake”. Kuna baadhi watakabiliana na Fumbo la kifo kwa mateso na mahangaiko makubwa, lakini daima wakiwa na maua ya matumaini ya ufufuko wa wafu!

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu ameipitia njia ya Fumbo la kifo na kufungua lango la matumaini ya ufufuko na uzima wa milele. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wale, Kristo Yesu amefungua lango la matumaini, linalowawezesha waamini kuingia ndani mwake, ili kulitafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ayubu anakiri kwamba, Mtetezi wake yu hai na atamwona na kulitafakari kwa kina Fumbo la huruma na upendo wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika mwezi huu wa Novemba, uliotengwa maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombesa Marehemu wote; kuwakumbuka kwani hawapo tena pamoja nao na kuanza pia kujiandaa kwa ajili ya safari inayoelekea kwenye maisha ya uzima wa milele, kwani Yesu mwenyewe anasema, atawafufua siku ya mwisho!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu na hatimaye kurejea tena mjini Vatican, alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusali na kuwaombea Mapapa waliotangulia mbele ya haki na kuzikwa chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.