2016-11-03 15:23:00

Dini ziwe ni tumbo la maisha ya binadamu na lango la matumaini!


Huruma ni thamani inayovuka mipaka ya Kanisa, inawaunganisha waamini wa dini mbali mbali kama sifa bora ya Mwenyezi Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kujikita katika majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, ili kutambua na kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma ni msingi thabiti wa Kanisa na ufunguo makini wa kuliangalia Fumbo la maisha ya binadamu ambaye leo hii ana kiu ya msamaha na amani!

Huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika upendo na huduma ya kidugu kwa kushirikishana. Kanisa linapenda kujielekeza zaidi katika mchakato huu, ili kukuza na kudumisha umoja na upendo kati ya watu! Dini mbali mbali zinahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: amani na umoja ili kutangaza na kushuhudia udugu unaopingana na vitendo vinavyoendelea kusababisha kinzani na baadhi ya watu kujifungia katika ubinafsi wao.

Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kujenga madaraja ya watu kukutana katika majadiliano yanayofumbata: ukweli na uwazi, ili kufahamiana na kuelewana vyema zaidi; kwa kufuta kiburi na udhalilishaji na hatimaye, kuondoa kila aina ya ukatili na ubaguzi. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 3 Novemba 2016 alipokutana na kuzungumza na wajumbe kutoka dini mbali mbali kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, dhamana kubwa iliyoko mbele ya dini mbali mbali ni kukuza na kudumisha umoja na upendo kati ya watu!

Tema ya huruma ya Mungu inafahamika katika dini na tamaduni mbali mbali kwa kuonesha huruma na msamaha; upendo na maisha; kwa kuthamini na kuendeleza utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala si bidhaa ya kuuzwa sokoni. Ni changamoto ya kuwa jirani na wale wote wanaopambana na magonjwa, udhaifu wa kibinadamu, umaskini, ukosefu wa haki; watu wanaoathirika kutokana na vita; wakimbizi na wahamiaji.

Dhamiri nyofu iwasaidie waamini wa dini mbali mbali kutoa msaada wa hali na mali kwa wahitaji zaidi kama kielelezo cha huruma ya Mungu ambaye, kamwe hawezi kuwatelekeza watoto wake kama anavyokaza kusema, Nabii Isaya. Waamini wawe na ujasiri wa kuondokana na matendo maovu kwa kushirikishana upendo unaopyaisha maisha. Binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko anayo kiu ya huruma ya Mungu, inayoweza kumfikisha katika bandari salama, mahali anapoweza kuona msahama na upatanisho, ili hatimaye kuondokana na hofu na wasi wasi inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamewawezesha waamini kwa unyenyekevu kupitia katika Lango la huruma, ili kupatanishwa na huruma ya Mungu inayowafutia dhambi zao, tayari hata wao pia kutoa msamaha kwa ndugu na jamaa waliowakosea, ili kwa pamoja waweze kushirikishana msamaha wa Mungu, ambao kimsingi ni gharama kubwa, lakini inayowawezesha kujisikia kuwa ni sawa na Mungu. Huruma ya Mungu inaambata pia mazingira, nyumba ya wote, changamoto kwa viongozi wa dini kusaidia kuelimisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira; kwa kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia; kwa kuzingatia pia ustawi na maendeleo ya wengi bila kugubikwa na ubinafsi.

Athari za mabadiliko ya tabianchi iwe ni changamoto ya kusimama kidete, kulinda na kutetea mafao ya wengi; kwa kujikita katika majadiliano yanayohitaji uvumilivu, ushiriki na ukarimu. Dini na wafuasi wake, ziwe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Lakini anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kusikitika kuona kwamba: vita, kinzani, utekaji nyara, mashambulizi ya kigaidi na uharibifu mkubwa wa mali za watu zinakuwa ni habari za kawaida.

Ni hatari kuhalalisha mashambuzi haya kwa kutumia jina la Mungu au dini fulani, mambo ambayo yanachafua maisha ya kiroho ya mwanadamu; waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani na uhuru wa kidini; dhamana na wajibu wao mbele ya Mungu, changamoto ya kushikamana kwa ajili ya mafao ya wengi. Dini ziwe ni tumbo la maisha ili kuendeleza upendo na huruma ya Mungu kwa ubinadamu uliojeruhiwa vibaya na unahitaji msaada; dini ziwe ni lango la matumaini, ili kuvuka kuta za kiburi na woga usiokuwa na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.