2016-11-02 08:47:00

Wakristo washikamane kujibu kilio cha walimwengu!


Ni jambo la furaha kubwa kutolea ushuhuda wa Roho wa Bwana kwa kuunganika pamoja wafuasi wa Kristo. Roho Mtakatifu ni Roho anayeita, anayekusanya, anayeangaza na kutakasa Kanisa zima la Kristo. Leo hii Roho Mtakatifu anauonesha muujiza wake tena katika tukio kubwa, ambapo Wakristo wote wanakusanyika kwa nguvu yake, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la kwanza mjini Yerusalem. Hii ni sehemu ya hotuba ya Askofu Munib Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri duniani, katika tukio la kiekumene nchini Sweden, Jumatatu [31 Oktoba 2016].

Askofu Younan anasema kuwa, mkusanyiko huo wa Kiekumene ni ushuhuda tosha kwamba, juhudi za pamoja za kidini zinaweza kujenga jamii ya amani na haki, na kutokomeza chuki na machafuko. Juhudi za kidini zinaposhiriki katika harakati za umoja na upatano, dini itanyanyua hali njema za jumuiya za wanadamu. Amesema kuguswa na ushuhuda uliotolewa na baadhi ya washiriki, kuhusu mahangaiko ya watu duniani, na kwamba kila mmoja anapaswa kuguswa, sababu kama afundishavyo Mtume Paulo: ndugu mmoja akipata mateso, jumuiya nzima hupata maumivu, na mmoja akiwa na mafanikio, ni furaha ya jumuiya nzima [Rej., IWakorintho 12:26]

Mabadiliko ya tabia nchi yanamuathiri kila mtu, kwa kuanzia na wanyonge zaidi. Kanisa lina nafasi kubwa ya kutetea haki za kijamii na jinsia katika tatizo la mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo kawaalika washiriki wote kutochoka wala kukaa kimya katika kutetea haki. Ameipongeza Serikali ya Colombia na wote walioshiriki katika kutafuta Amani na wapiganaji wa msituni guerrillas. Kawaalika wananchi wote wa Colombia kuipa sasa nafasi Amani itawale nchini mwao, ili watu waishi kwa haki na kwa kuheshimu utu wa mwanadamu. Kwa sababu hiyo wasiipe tena nafasi biashara ya silaha.

Askofu Younan kawatia moyo pia wakimbizi wa Burundi na Kenya kuendelea kuombea Amani na kushiriki kadiri ya nafasi katika kujenga Amani ya kudumu, katika maeneo yao na dunia nzima. Askofu Younan amesimulia kwamba yeye pia ni mkimbizi wa kipalestina, na wazazi wake wanatokea Beer Sheva. Akisimulia kumbukumbu za nyakati za nyuma, kawashukuru jumuiya ya Kiinjili ya kilutheri iliyotenda utume Yerusalemu na kuwasaidia wakimbizi wengi wakati akiwa mkimbizi. Katoa mwaliko kuendelea kujali wakimbizi na kuhakikisha wanapata kila mahitaji na kila furaha kwa kuheshimu pia utu wa kila mmoja.

Ameelezea kwamba, pamoja na ukweli kuwa haombei Wakristo kufa mashahidi, bado anawatia moyo wote wanaoishi katika jumuiya ambamo Wakristo wanateswa, wazingatie ujumbe wa Kristo anayewaalika wasiogope [Rej., Luka 12, 32]. Amewaalika wote kutotulia mpaka Amani itawale duniani. Makanisa kwa kushirikiana na wote wenye mapenzi mema, watetee haki na kuhangaikia Amani. Kawaalika pia kuombea Israeli ili Wapalestina na Wayahudi waweze kuishi kwa Amani, na dini za Kikristo, Kiislamu na Kiyahudi waishi kama ndugu nchini Israeli.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.