2016-11-02 08:35:00

Wakristo waguswe na mahangaiko, furaha na matumaini ya walimwengu!


Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri duniani, kawakaribisha washiriki katika tukio la Kiekumene nchini Sweden, akiwakumbusha jukumu lao la msingi la kuushuhudia Umoja wa Kiekumene duniani. Sala za pamoja za ufunguzi zilizoelekezwa kuachana na tofauti na mafarakano, na badala yake kusonga mbele kwa pamoja, wakiitikia wito wa Mungu wakuwa wamoja, zimekuwa sala za kutambua makosa ya kale na kutubu, kuombea uponyaji wa ndani kwa kila mmoja na hivyo kuthibitisha utayari wa kushuhudia umoja wao.

Dr. Junge kawaalika washiriki kuguswa na mateso na maumivu, lakini pia furaha na matumaini ya watu duniani. Ni katikati ya uhalisia huu wa dunia ya leo, ambapo umoja na mshikamano wa Makanisa unahitajika kutolea ushuhuda. Ujumbe wa uzima tele, haki, amani na mapatano ni ujumbe ambao hauwalengi wale tu waliokusanyika katika tukio hilo la Kiekumene Sweden, bali ni ujumbe ambao wanapaswa waubebe na kuufikisha katika kila kona ya dunia, dunia ambayo Mungu aliipenda kiasi cha kumtuma Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo, kwa ajili ya kuikomboa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.