2016-11-02 09:04:00

Ushuhuda wa Uekumene wa huduma!


Wakati Mkutano wa Kiekumene ukiendelea huko Sweden, kumetolewa ushuhuda na baadhi ya washiriki siku ya Jumatatu [31 Oktoba 2016]. Pranita Biswasi binti mwenye umri wa miaka 26 kutoka India, ameeleza kuwa eneo analotoka, zaidi ya watu bilioni 1.3 wanaishi katika hali duni sana ya maisha. Kuna wachache wanaoishi katika utajiri mkubwa na wengi wakihangaika kupata lishe ya siku. Eneo hilo la Kusini Mashariki mwa India wanakumbana na majanga mengi asilia, vimbunga, mafuriko, ukame na hivyo wakulima wengi kuathirika.

Ana shahada ya pili katika Sayansi ya mazingira, elimu iliyomsaidia Pranita kuelewa kwamba mabadiliko ya tabia nchi, yana athari kubwa kwa dunia. Mwaka 2013 na mwaka 2015, India imepatwa na majanga ya mafuriko yaliyopelekea zaidi ya watu 500 kupoteza maisha na takribani milioni 1.8 kuhama nyumba zao. Wengi wamejiua kwa kukata tamaa ya maisha au wakulima kushindwa kulipa madeni ya mikopo waliyochukua, wakitegemea kuwekeza katika kilimo. Kwa kuona jinsi watu wanavyoteseka, Pranita aliamua kujiunga na shughuli za kutetea haki za watu katika mabadiliko ya tabia nchi. Kwa sasa anaifurahia shughuli hiyo katika Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani. Pranita anawaalika Waluteri na Wakatoliki kwa pamoja, kuunganisha nguvu kutetea haki za maskini wengi wanaoteseka. Ingawa kuna juhudi nyingi katika mataifa kutatua changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, bado kuna tofauti kubwa kati ya hali ya sasa na malengo ambayo wanadamu wangependa kuyafikia.

Monsinyo Heector Gaviria, Mkurugenzi wa CARITAS nchini Colombia, kaeleza kuwa ni tamaduni ya watu wa Marekani ya kusini kuchapa kazi kwa bidii, hata hivyo mgawanyiko wa kijamii na siasa za utengano, zimepelekea machafuko maeneo hayo. Katika makovu ya kihistoria ya Colombia ni pamoja na mauaji ya 2002 ambapo mamia ya wakimbizi waliopata hifadhi katika Kanisa moja, waliuawa kwa bomu. CARITAS nchini Colombia imefanya kazi kubwa katika kujenga upya maisha ya watu na jumuiya zao, na urejeshwaji wa haki zao.

Juhudi za Kanisa nchini Colombia zimesaidia mazungumzano kati ya serikali na wapiganaji wa kikundi cha waasi cha guerrillas, yaliyoanzia nchini Cuba na mwaka huu Septemba 26, wamefanikiwa kutia saini ya makubaliano. Katika eneo lingine la Colombia inapopakana na Venezuela, wakulima na wananchi wengi wamepoteza maisha na kunyanyaswa kutokana na vikundi vilivyo kinyume na wachimbaji wadogo wa madini. Kwa eneo hili, Kanisa Katoliki limeshirikiana vema na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri katika kujibu kilio cha wananchi wengi wa eneo hili, wanaohitaji ulinzi. Kamshukuru pia Baba Mtakatifu Francisko kwa ushiriki wake katika kutafuta Amani nchini Colombia.

Marguerite Barankitse wa Burundi kasimulia namna alivyowaficha na kuwatunza watoto zaidi ya 30, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Kupitia Nyumba ya Amani [Maison Shalom] walipowatunza watoto hao, walifanikiwa kuvunja mnyororo wa chuki na kutengeneza kizazi kipya cha upendo. Kwa hakika walikuwa mshumaa unaowaka kati ya giza.  Watoto hao wa miaka 23 iliyopita, leo hii wana familia zao na wametengeneza umoja wa kusaidia wahitaji. Hata leo hali ni hatari maeneo hayo, hivyo wanalazimika kukimbilia Rwanda na kuwatunza wakimbizi huko.

Rose Lokonyen ni mkimbizi aliyeshiriki katika Timu ya michezo ya wakimbizi katika michezo ya Olympic mwaka huu 2016. Rose ni binti wa Sudan ya kusini na ana umri wa miaka 23, amekuwa mkimbizi nchini Kenya tangu akiwa na miaka 8. Akiwa na umri wa miaka 14 wazazi wake walirudi Sudan ya Kusini kuwatafuta bibi na babu zao, lakini toka hapo hana tena mawasiliano na wazazi wake, na hajui nini kiliwapata. Akiwa mtoto mkubwa ilibidi aanze kuwatunza wadogo zake kwa kufanya kila kazi za nyumbani, huku akiendelea na masomo.

Rose ni mpenda michezo na amekuwa akitenga muda kila siku jioni kufanya michezo. Katika eneo la kambi ya wakimbizi, Rose anashiriki kuwashawishi vijana kupenda kusoma na kuwa makini na magonjwa hatari kama Ukimwi. Rose Kaomba watu wote waelewe kuwa wakimbizi wanahitaji sio chakula na malazi peke yake, bali wanapenda kukua na kushirikishwa shughuli mbali mbali za jamii ili kujisikia kweli nao wana thamani katika maisha. Ameiomba Jumuiya ya Kimataifa kuungana na kutatua tatizo la vita na machafuko duniani. Kawaalika wajumbe wa Kiekumene kuendelea kuombea Amani duniani.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.