2016-11-02 06:48:00

Heri za Mlimani ni utambulisho na muhtasari wa mafundisho ya Yesu


Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Sweden, tarehe 1 Novemba, 2016 Siku kuu ya Watakatifu wote, imebahatika kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwepo nchini Sweden kwa ziara ya siku mbili ya kiekumene. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, Siku kuu ya watakatifu ni kumbu kumbu endelevu si tu kwa waamini ambao majina yao yameandikwa kwenye Orodha ya watakatifu, bali hata wale Wakristo ambao wamejitahidi kuishi kikamilifu upendo na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika hali ya kawaida.

Hii ni siku kuu ya utakatifu wa maisha ya Kikristo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha mintarafu dhamana ya Ubatizo. Ni utakatifu unaofumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani; upendo unaomwajibisha mwamini kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine. Heri za mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo na lengo la kila mwamini. Huu ni mwongozo na dira ya maisha inayooneshwa na Kristo, ili wafuasi wake, waweze kufuata nyayo zake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Heri za mlimani ni utambulisho  wa Kristo Yesu na ni utambulisho wa Mkristo. Kwa namna ya pekee amependa kukazia  wito wa Yesu kwa wafuasi wake, anaowaalika kujifunza kutoka kwake, kwa kuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Huu ndio utambulisho wa Yesu kiroho na kielelezo cha utajiri wa upendo wake. Unyenyekevu ni kielelezo cha fadhila kinachomtambulisha mtu jinsi alivyo na anavyoishi kwa kumkaribia Kristo Yesu na kuwawezesha kuwa na umoja kati yao.

Hii ni changamoto na mwaliko wa kuacha yote yanayowatenganisha na kuambata mambo msingi yanayowaunganisha, kama walivyofanya na kutenda watakatifu kutoka Sweden waliotangazwa na Mama Kanisa hivi karibuni, kati yao ni Mtakatifu Elizabeth Hesselblad; Mtakatifu Brigida na Mtakatifu Briditta Vadestena, wasimamizi wenza wa Bara la Ulaya. Hawa ni watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, umoja na mshikamano vinajengwa na kudumishwa na Wakristo, katika nchi ambamo kuna Makanisa mengi.

Hii ni alama muhimu sana katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Watakatifu wanaweza kuambata mageuzi kutokana na unyenyekevu wa moyo, kielelezo cha ukuu wa Mungu; mwaliko wa kumwabudu katika ukweli bila kuogopa jambo lolote, kwani hawana kitu ambacho wanaweza kupoteza, wana  uhakika kwamba Mungu ndiye kisima cha utajiri wao.

Heri za Mlimani anaendelea kusema Baba Mtakatifu ni kitambulisho cha mfuasi wa Kristo Yesu. Waamini wanaalikwa na kuhamasishwa kuwa ni wenyeheri kwa kupambana na machungu na hofu za maisha ya duniani kwa moyo na upendo wa Yesu, ili kuwaonesha walimwengu mwelekeo mpya wa maisha. Heri wanaovumilia kwa imani mateso na mahangaiko wanayokabiliana nayo na kusamehe kutoka katika undani wa mioyo. Heri wanaowaangalia watu wanaoteseka kutokana  na sababu mbali mbali na wako tayari kuwaonjesha uwepo wao wa karibu; heri wale wanaomtambua Mungu kwa kila mtu na wanasimama kidete ili kuwasaidia wengine kuitambua na kuenzi sura na mfano wa Mungu kwa watu hawa.

Heri wanaolinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote: Heri wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao na ustawi wa wengi; heri wanaosali na kujisadaka kwa ajili ya umoja kamili wa Wakristo. Watu wote hawa anasema Baba Mtakatifu ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu na watapata tuzo wanayostahili. Wito na mwaliko kwa utakatifu wa maisha ni kwa ajili ya wote pasi na ubaguzi, changamoto ni kuupokea mwaliko huu kwa moyo wa imani. Watakatifu wanawatia shime waamini kwa njia ya mifano ya maisha na sala zao, kuwa watakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kupokea wito huu wa utakatifu wa maisha na kuendelea kushikamana ili uweze kufikia utimilifu wake. Bikira Maria Malkia wa watakatifu wote awasaidie waamini kutekeleza nia hii njema pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuwa na umoja wa wakristo wote na hatimaye nguvu hizi zisaidie ujenzi wa utakatifu wa umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.