2016-10-31 15:41:00

Papa Francisko hii ni hija ya kikanisa na kiekumene!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 31 Oktoba 2016 ameanza hija yake ya kitume ya 17 nchini Sweden ambako anashiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani pamoja na kutembelea Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo. Hii ni hija inayojikita katika majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Jumatatu ni siku ambayo imefumbata matukio makuu mawili yaani Ibada ya pamoja kwenye Kanisa kuu a Lund pamoja na sherehe ya shuhuda mbali mbali za Uekumene wa huduma kati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis na Shirikisho la Huduma la Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani zinazofanyika kwenye Uwanja wa michezo wa Malmo.

Jumanne, Siku kuu ya Watakatifu wote, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jumuiya ya Wakatoliki nchini Sweden. Itakumbukwa kwamba, Sweden kunako mwaka 1989 alimpokea Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi hii kubwa na muhimu. Amewakumbusha kwamba, hii ni hija ya kikanisa na majadiliano ya kiekumene. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kamba, huduma yao, itawasaidia watu kutambua vyema tukio hili la kihistoria katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Sweden ametuma salam na ujumbe wa matashi mema kwa wakuu wa nchi ya: Italia, Austria na Ujerumani. Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Rais Sergio Mattarella wa Italia akisema, anakwenda nchini Sweden ili kushiriki katika maadhimisho ya kiekumene ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani pamoja na kukutana na Jumuiya ya Wakatoliki nchini Sweden. Amemwomba, Rais Mattarella pamoja na familia ya Mungu nchini Italia, kumsindindikiza katika hija hii ya kitume na kwamba, anawatakia ufanisi mwema katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Rais Doris Bures wa Baraza la Kitaifa la Austria amewatakia: amani, ustawi na maendeleo wananchi wote wa Austria. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Rais Joachim Gauck wa Ujerumani amewatakia heri na baraka; amani na ustawi kwa wananchi wote wa Ujerumani. Baba Mtakatifu alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malmo amepokewa na Bwana Stefan Lovfven Waziri mkuu wa Sweden aliyekuwa ameambatana na  Bi Alice Bah-Kuhnke, Waziri wa Utamaduni na Demokrasia pamoja na viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, waliokuwa wamesindikizana na Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Sweden.

Baada ya mapokezi haya ya kitaifa, Baba Mtakatifu alipata chakula cha mchana kwa faragha. Lakini waziri mkuu wa Sweden aliandaa chakula cha mchana kwa ujumbe wa Vatican uliongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, liliandaa pia chakula cha mchana kilichowajumuisha wajumbe wote wa kiekumene wanaohudhuria tukio hili la kihistoria! Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko alipata mapumziko mafupi kabla ya kuingia kwenye kiini cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani huko Lund, nchini Sweden. Lakini kabla ya tukio hili, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea Familia ya Mfalme Carl Gustav XVI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.